1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masai Mara

16 Desemba 2008

Mbuga ya wanyama ya Masai Mara nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/GHMn

Mbuga za Taifa nchini Kenya, ni kivutio kikubwa kwa watalii wanaotembelea Kenya ili kufurahia mazingira na maumbile ya bara la Afrika kwa macho yao.

Chemchem hii inayochangia mno mfuko wa fedha za kigeni kutokana na utalii sasa inahatarishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.tayari leo watu wanahofia kupoteza kazi zao .

Ndani ya gari la aina ya "Rangerover" msafara unapita katika mbuga za Taifa za Masai Mara.Dereva anaelewa wapi simba,twiga na tembo walipo.

kikundi kizima cha wanayma hao kimepiga maskani yao kwenye mbuga huku jua likikaribia kutua.Lakini sura hii ya utulivu na amani, imeingia ufa.Rufus Kimani,meneja wa mojawapo ya kambi za safari, anahofia athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika biashara ya utalii.Anasema ukame unaongezeka.

"Ikiwa hali ya hewa itaendelea kuchafuka zaidi, basi tutakabiliwa na mabadiliko makubwa upande wa safari za kitalii.Wageni wetu hawatajionea tena sura hii ya leo kwavile aina mbali mbali za wanyama zitatoweka.Vipindi vya ukame vitazidi-hali itazidi kuharibika. "

"Kichwa Tembo" ni jina la "safari-hoteli" ambako mlinzi wake anaewakaribisha wageni kinapoingia kiza nyakati za magharibi ni Mmasai: Wakaazi wa eneo karibu na hoteli hiyo hunufaika na utalii na sasa umo hatarini-anasema Kimani.Masai mara ni maarufu kwa kupita hapo hadi pundamilia na kongoni milioni 2 wanaovuka mto Mara.

Daniel Oma mlinzi wa kambi hiyo anasema:

"Wanyama hao wanapita Masai mara kila mwaka na kwa desturi huja mwezi julai wakitokea Serengeti.Hapo eneo zima huzagaa wanyama hao na hasa kongoni na pundamilia- kiasi cha kongoni milioni 1.5 na pundamilia 200.000

hupita hapo.Halafu huwasili aina mbali mbali ya paa.ni sura ya kuvutia ajabu."

Watalii wanalipa fedha nyingi ili kuangalia mkusanyiko huo.Kima cha chini kwa siku moja katika hoteli ya kifahari ni dala 200.

Watalii lakini, wanazidisha nao tatizo la uharibifu wa mazingira katika Masai Mara-wanaonya wataalamu wa kisayansi.Kila mgeni anatumia lita 400 za maji kila siku na hii- ni kwa muujibu wa taftishi zilizofanywa na wataalamu wa kimarekani na shirika la kutunza mbuga (WWF.)

Utalii nchini kenya bado haukurudi kustawi baada ya machafuko ya mapema mwaka huu wa 2008.Hii ina maana kuwa, mazingira hayakuchafuka sana ,lakini kwa upande mwengine, fedha zinakosekana kwa shughuli za kupiga doria ili kuwalinda wanyamapori. Mashirika ya kutunza wanyamapori na mazingira mfano wa WWF, yanajionea hatari hapo ya kudhurika wanyama.

Isitoshe,kuzidi kwa ukame nako kunaongezea shida ya chakula ya wakaazi na hivyo hatari ya kuwawinda wanyama.Rufus Kimani kwahivyo, ana wasi wasi kuwa mbuga ya Taifa ya Masai Mara, siku zijazo haitamudu kuvumilia misuko suko kama hiyo.