1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marudio ya uchaguzi chini ya ulinzi mkali Zanzibar

20 Machi 2016

Visiwa vya Zanzibar vyenye mamlaka ya ndani nchini Tanzania Jumapili (20.03.2015)chini ya ulinzi mkali vimekuwa na marudio ya uchaguzi uliosusiwa na chama kikuu cha upinzani cha CUF.

https://p.dw.com/p/1IGae
Mwananchi akipiga kura katika kituo cha Mji Mkongwe Zanzibar. (20.03.2016)
Mwananchi akipiga kura katika kituo cha Mji Mkongwe Zanzibar. (20.03.2016)Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa awali hapo tarehe 25 mwezi wa Oktoba kwa madai ya udanganyifu.Lakini wanadiplomasia wamesema hawakuona ushahidi wowote ule wa kuwepo kwa udanganyifu mkubwa unaodaiwa kutokea.

Chama kikuu cha upinzani (CUF) kimesema kilikuwa kimeshinda uchaguzi huo na kimeonya juu ya uwezekano wa kuzuka ghasia katika visiwa hivyo vya bahari ya Hindi iwapo uchaguzi huo ungeliendelea kufanyika Jumapili.

Chama cha CUF kimewahimiza wafuasi wake kuususia uchaguzi huo wa rais,wawakilishi na serikali za mitaa jambo linalomaanisha ushindi bwerere kwa chama tawala cha CCM.

Vyama vingine vidogo vinashiriki uchaguzi huo lakini uchaguzi visiwani Zanzibar kwa kawaida unakuwa wa ushindani mkali kati ya CCM na CUF.

Usalama waimarishwa

Hali ya usalama ilikuwa imeimarishwa kwenye vituo vya kupigia kura.Chaguzi za nyuma visiwani humo zilikuwa zimechafuliwa na vurugu.

Mpiga kura katika kituo cha Mji Mkongwe Zanzibar. (20.03.2016)
Mpiga kura katika kituo cha Mji Mkongwe Zanzibar. (20.03.2016)Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Takriban vituo vingi vya kupigia kura vilikuwa vimefunguliwa kwa wakati hapo saa moja asubuhi ambapo wapiga kura waliunda misururu kwa amani lakini idadi ya walijotokeza kupiga kura inaonekana ni ndogo katika ngome za CUF ambapo wafuasi wa chama hicho wameitikia wito wa chama chao kuususia uchaguzi huo.

Mfuasi wa chama tawala CCM ambacho kinaunga mkono marudio hayo ya uchaguzi Amina Hassan amesema " Nina furaha kupiga kura tena. Tutapata ushindi wa vishindo "

Mwanachama wa upinzani Yussuf Juma ameupuzilia mbali uchaguzi huo kuwa ni wa kiini macho.Amekaririwa akisema "Ni kupoteza wakati na rasilmali kupiga kura tena.Tumewasikiliza viongozi wetu waliotutaka tusipige kura na tumeamu kuususia."

Kauli ya Shein

Rais anayetetea wadhifa wake Ali Mohamed Shein alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kupiga kura katika kituo kilioko Mji Mkongwe mji mkuu wa Zanzibar ambao ni wa kihistoria.

Rais anayetetea wadhifa wake Ali Mohammed Shein.
Rais anayetetea wadhifa wake Ali Mohammed Shein.Picha: DW/M. Khelef

Shein amesema ana furaha kutumia haki yake ya kidemokrasia na kuongeza "sio sahihi kwa upinzani kususia lakini wana uhuru wa kufanya hivyo."

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imesema kumekuwa hakuna ucheleweshaji katika kuwasilishwa kwa visanduku na makaratasi ya kupigia kura na kwamba waangalizi wa uchaguzi wa ndani ya nchi na wale wa Afrika wako mahala pao isipokuwa wale wa Umoja wa Ulaya ambao hawakushiriki.

Kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba visiwani Zanzibar kumekuja baada ya mgombea wa CUF Seif Sharrif Hamad kujitangaza mshindi kabla ya matokeo kutangazwa rasmi.

Nia kuinyima CUF ushindi

Viongozi wa CUF wamesema hatua hiyo ilikuwa imesanifiwa ili kuzuwiya ushindi wa chama chao na kuipatia ushindi mwengine CCM ambacho kinahodhi madaraka Tanzania bara.

Katibu Mkuu wa chama cha CUF Seif Sharif Hamad.
Katibu Mkuu wa chama cha CUF Seif Sharif Hamad.Picha: DW/M. Ghassani

Serikali ya Zanzibar ilipiga marufuku kwa muda usafiri wa baharini kati ya visiwa hivyo na Tanzania bara hapo Jumapili kwa kile maafisa wa serikali walichosema ilikuwa ni hatua iliokusudia kuhakikisha kwamba uchaguzi huo hauvurugwi.

Takriban wapiga kura 500,000 visiwani Zanzibar walikuwa pia wakistahiki kupiga kura zao katika uchaguzi wa Oktoba kumchaguwa rais wa Tanzania na licha ya kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar,Rais mpya wa Tanzania John Magufuli aliapishwa mwaka jana.

Vituo vya kupigia kura vinatazamiwa kufungwa saa kumi jioni na matokeo yanatarajiwa kutolewa hata Jumatatu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mwandishi : Isaac Gamba