1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marsabit: Wamiliki wa bunduki haramu wapewa muda kuzirudisha

Michael Kwena3 Agosti 2020

Serikali ya Kenya imetangaza msahama kwa wanaomiliki bunduki haramu katika jimbo la Marsabit watakaozirejesha kwa hiari katika muda wa miezi miwili.

https://p.dw.com/p/3gKWO
BG Kenia Turkana Kriger
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na ongezeko la silaha haramu katika jimbo hilo ambalo limeendelea kushuhudia visa vya uhalifu na mapigano ya kikabila kwa kutumia bunduki.

Jimbo hilo la mpakani ambalo idadi kubwa ya wakaazi wake ni wafugaji, limeripoti ongezeko la silaha haramu ambazo zimekuwa zikitumiwa kufanya uhalifu na pia kuchangia katika mapigano ya kikabila ambayo sasa yamekuwa jambo la kawaida.

Kwa mujibu wa tume ya maridhiano nchini NCIC, wakaazi kwenye mpaka huu wa Kenya na Ethiopia, wamekuwa wakijihami kwa bunduki kwa kile NCIC imetaja kuwa, inatokana na wakaazi hao kukosa imani na asasi za kiserikali zenye jukumu la kuwapa ulinzi.

Kamishna wa tume hiyo Dakta Danvas Makori katika ziara yake Marsabit, aliitaka serikali kuwajibika kwa kuwakamata wanaofanya uhalifu na kuwafikisha katika mahakama kama njia itakayosaidia kumaliza migogoro ya kila mara

”Silaha haramu ni nyingi sana upande wa kaskazini mwa Kenya na kuna takriban silaha haramu laki saba.Kabla zitwaliwe,serikali ni lazima iwahakikishie usalama kwa sababu,watu walijihami kwa silaha kwa sababu walihisi serikali haiwezi kuwalinda,” amesema Makori.

Muda wa msamaha kufuatwa na operesheni ya maafisa wa usalama

Mnamo Machi 24, 2010, Kenya iliteketeza moto bunduki haramu 2,545 zilizisalimishwa kwa hiari pamoja na zilizopatikana baada ya msako wa walinda usalama
Mnamo Machi 24, 2010, Kenya iliteketeza moto bunduki haramu 2,545 zilizisalimishwa kwa hiari pamoja na zilizopatikana baada ya msako wa walinda usalamaPicha: AP

Wakati huohuo, serikali imetangaza msamaha wa miezi miwili kwa watakaorejesha bunduki zao kwa idara ya usalama.

Kulingana na kamishana wa jimbo la Marsabit Evans Achoki, baada ya kukamilika kwa muda huo, serikali itazisaka bunduki zote haramu na kuwakabili kwa mujibu wa sheria watakaopatikana nazo.

"Tumefaulu kupata mamia ya bunduki haramu na tutaendelea kuzisaka nyingine. Mwezi huu wa nane na tisa, ni mwezi wa msamaha kwa wanaomiliki bunduki haramu na baada ya muda huo kukamilika, tunatajia kwamba, watu wegi watakuwa wamerejesha silaha hizo,” amesema Achoki.

Wakaazi katika jimbo la Marsabit, wamekuwa wakinunua bunduki katika taifa jirani la Ethiopia kwa bei nafuu duru zikiiarifu DW kwamba, bastola moja inanunuliwa kwa shilingi elfu thelathini nchini humo.

Idara ya usalama kwa upande wake, imesema imeziba mianya kwenye mpaka wake na Ethiopia na hivyo wakaazi hawatafaulu kuvuka upande wa pili kununua bunduki hizo.

Serikali imesema msamaha huo ndio wa mwisho kutolewa kwa wakaazi wa Marsabit kusalimisha bunduki. Muda huo ukikamilika, wale ambao hawatakuwa wamesalimisha bunduki zao watakabiliwa bila huruma.

Mwandishi: Michael Kwena,DW Marsabit

Mhariri: Gakuba, Daniel