1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yazungumza na washirika wake pamoja na Urusi kuhusu mpango wa kutanua ulinzi wake Ulaya

19 Aprili 2007

Urusi ina wasi wasi na uwekaji mfumo wa ulinzi huko Poland na Cheki zilizo karibu na mipaka yake.

https://p.dw.com/p/CHFt
Makao makuu ya NATO Brussels
Makao makuu ya NATO BrusselsPicha: NATO

Marekani leo imeimarisha juhudi zake za kumaliza hasira za Urusi na washirika wake wenye wasi wasi barani Ulaya, kuhusu mipango yake ya kutanua mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora barani Ulaya.

Akizungumza kabla ya mkutano pamoja na Urusi na waakilishi wake Marekani katika Jumuiya ya kujihami ya magharibi-NATO, Mkurugenzi wa wakala wa unaohusika na ulinzi wa makombora , alisema kwamba makakati wa kinga ya aina hiyo unahitajika ili kuizuwia Iran na mataifa mengine katika mashariki ya kati kuwa na uwezo wa kutengeneza makombora ya masafa marefu, yanayoweza kuwa kitisho kwa Ulaya au Amerika kaskazini.

Luteni Jenerali Henry A. Obering aliuambia mkutano na waandishi habari nchini Poland kabla ya mazungumzo ya leo mjini Brussels kwamba mataifa kama Iran, Syria na mengineyo yanaziona silaha hizi kama muhimu kwa sababu kihistoria hakujapata kuwa na kinga dhidi ya silaha hizo. Lakini sasa imefikiwa hatua ya kuwa na mfumo wa kujilinda dhidi ya silaha hizo.

Luteni Jenerali Obering na Naibu waziri wa ulinzi wa Marekani anayehusika na sera Eric Edelman watawaarifu washirika wa Marekani pamoja na maafisa wa Urusi katika makao makuu ya NATO mjini Brussels juu ya mpango huo wakijaribu kuondoa hofu iliopo kwamba Marekani ina azma ya kujitanua kijeshi barani Ulaya na hasa karibu na mipaka ya Urusi, na tayari kabla ya mutano wao walikua na mazungumzo na Katibu mkuu wa NATO Jaap de Hoop Scheffer.

Urusi imeulaani mpango huo wa kutaka kuweka mfumo wa kujikinga dhidi ya makombora nchini Poland na mitambo ya uchunguzi ya rada katika Jamhuri ya Cheki.Naibu waziri mkuu wa Urusi Sergei Ivanov amesisitiza katika mahojiano na gazeti la Financial Times la mjini London kwamba Iran haiwezi kuwa na uwezo wa kutengeneza makombora ya kutoka bara moja hadi jengine kwa siku za usoni, kinyume na Marekani inavyodai.

Ujerumani imedai paweko na mashauriano ya karibu na Urusi, lakini hata nayo pia imekua na wasi wasi juu ya mpango huo. Baadhi ya wadadisi katika makao makuu ya NATO wanaashiria kwamba, huenda Marekani inataka kuharakisha mpango wake huo, kabla rais wa sasa George W. Bush hakumaliza muda wake madarakani hapo mwaka ujao.