Marekani yathibitisha kufikia makubaliano na Taliban | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.02.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Afghanistan

Marekani yathibitisha kufikia makubaliano na Taliban

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema nchi yake itatiliana saini na kundi la Taliban tarehe 29 mwezi huu juu ya kusimaisha mapigano nchini Afghanistan

Makubaliano hayo yatatiwa saini mbele ya wasimamizi wa kimataifa baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya wajumbe wa Umoja wa Falme za kiarabu,Taliban na Marekani. Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid pia amefahamisha kwamba Marekani na Taliban watafanya mipango juu ya kubadilishana wafungwa wa kivita.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Pompeo ameeleza kuwa pande mbili hizo zimekuwa zinafanya mazungumzo kwa lengo la kuleta suluhisho la kisiasa na pia amefahamisha kwamba Marekani itapunguza idadi ya askari wake nchini Afghanistan.

Mkataba kati ya Marekanai na Taliban utatiwa saini kutegemea na hatua zitakazochukuliwa ili kupunguza mapigano nchini Afghanistan kote kwa kiwango kikubwa. Mkataba huo utatoa fursa ya kuleta amani baada ya miaka mingi ya vita na uwepo wa majeshi ya Marekani tangu mwaka 2001.

Katibu Mkuu wa mfungamano wa kijeshi wa NATO Jens Stoltenberg kwenye taarifa yake amesifu mkataba huo kuwa utafungua njia ya kuleta amani ya kudumu. Amesema hatua hiyo inaweza kufungua njia ya mazungumzo kati ya Waafghanistan na hatimae kuhakikisha kuwa nchi hiyo sio tena mahala salama kwa magaidi.

Mbele: Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo. Nyuma: Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani

Mbele: Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo. Nyuma: Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani.

Wajumbe wa Marekani na Taliban wamekuwa wanafanya mazungumzo kwenye mji wa Doha tangu mwaka 2018 katika muktadha wa mapigano ambapo wapiganaji wa Taliban waliimarisha mapambano na kuweza kuyadhibiti maeneo zaidi ya nchi ya Afghanistan.

Maalfu ya raia na askari waliuawa. Kulingana na msemaji wa serikali ya Afghanistan hatua ya kupunguza mashambulio kati ya Taliban, majeshi ya kimataifa na majeshi ya serikali ya Afghanistan itaanza kutekelezwa kwa muda wa wiki moja. Msemaji huyo amesema anatumai kuwa muda huo utarefushwa na kufungua njia ya kusimamisha mapigano na kufanyika mazungumzo kati ya Taliban na serikali ya Afghanistan. 

Viongozi waandamizi watatu wa Taliban wamethibitisha mjini Doha na nchini Afghanistan kwamba wamekubaliana juu ya kupunguza mashambulio kwa muda wa siku saba kuanzia Ijumaa. Hata hivyo kiongozi mmoja wa Taliban mjini Doha amesema makubaliano hayo hayawezi kuitwa ni hatua ya  kusimamisha mapigano kwa muda. Ameeleza kwamba kila upande unayo haki ya kujihami lakini amesema katika kipindi hicho cha  wiki moja, hakuna upande utakaofanya mashambulio dhidi ya mwingine. Ameongeza kwa kueleza kwamba lengo ni kujenga mazingira ya usalama nchini Afghanistan na kwamba kipindi cha amani kinaweza kurefushwa ikiwa mambo yataenda vizuri baada ya mktaba wa amani kutiwa saini na Marekani.

Vyanzo:/AP/AFP/RTRE/DPA