1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Antony Blinken yuko ziarani Mashariki ya kati

Saumu Mwasimba
25 Mei 2021

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameahidi nchi yake itasaidia kuijenga upya Gaza baada ya vita vya siku 11 vilivyouharibu mji huo wa pwani

https://p.dw.com/p/3tw7S
Israelisch-palästinensischer Konflikt : US-Außenminister Blinken zu Besuch in den Nahen Osten
Picha: Menahem Kahana/UPI Photo/Imago Images

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameahidi msaada wa nchi yake katika ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza, ingawa amesisitiza kwamba msaada huo haupaswi kuwafaidisha Hamas, kundi ambalo linashikilia mamlaka ya ukanda huo wa Gaza.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ametoa tamko hilo la nchi yake kuisaidia  Gaza baada ya kukutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu,na tangazo hilo ni sehemu ya lengo lake la ziara ya Mashariki ya kati itakayoendelea hadi siku ya alhamisi,ambalo ni kusaidia usitishaji mapigano baina ya Israel na maeneo ya wapalestina.

Gaza nach den Bombenangriffen Israels
Picha: Tania Kraemer/DW

"Rais Biden ameniomba nije hapa leo kwa sababu nne. Kwanza ni kuonesha kujitolea kwa Marekani katika usalama wa Israel, kuanza kufanya kazi kuelekea uthabiti mkubwa na kupunguza mivutano katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, kusaidia kutoa msaada wa dharura wa kibinadamu na ujenzi mpya wa Gaza na kuendelea kujenga tena uhusiano wetu na watu na mamlaka ya wapalestina.''

Blinken ameahidi kuihamasisha jumuiya ya kimataifa kutoa mchango wa kuisadia Gaza kufuatia vita vibaya vilivyoliharibu kabisa eneo hilo. Lakini pia mwanadiplomasia huyo amesema hatua hiyo itachukuliwa kwa kuhakikisha upande mwingine kwamba msaada huo haungii mikononi mwa kundi la Hamas ambalo ndio watawala wa Gaza.

Blinken  ambaye amepangiwa kukutana na rais wa mamlaka ya wapalestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah huko Ukingo wa Magharibi baadae leo amesisitiza pia kwamba mivutano katika ukingo huo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki inahitaji kupunguzwa na kuupigia upatu kurudishwa uhusiano na mamlaka ya wapalestina. Mwanadplomasia huyo wa ngazi za juu wa Marekani pia anapanga kukutana na rais wa Misri Abdel Fatah al Sisi na mfalme Abdullah ii wa Jordan mnamo wiki hii.

Israelisch-palästinensischer Konflikt : US-Außenminister Blinken zu Besuch in den Nahen Osten
Picha: Alex Brandon/AP Photo/pciture alliance

Vita vya siku 11 baina ya Israel na Hamas vilisababisha kuuwawa watu 250 wengi walikuwa ni Wapalestina na kusababisha uharibifu mkubwa sana katika eneo hilo masikini la pwani la Gaza.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalianza kutekelezwa tangu ijumaa iliyopita na mpaka sasa yanatekelezwa japo makubaliano hayo hayakugusia kabisa masuala yoyote ambayo ndio chachu ya mgogoro huo wa Israel na Wapalestina,jambo ambalo  Blinken amekiri baada ya kukutana na Netanyahu.

Blinken amesema anafahamu ili kuepusha machafuko kutokea tena wanapaswa kutumia nafasi iliyopo kushughulikia sehemu kubwa ya masuala ambayo ni chachu ya mgogoro na changamoto zilizopo.Lakini pia akaongeza kusema Marekani inaamini Israel na Wapalestina wote wanahaki sawa ya kuishi  kwa usalama,kufurahia hatua sawa za uhuru na fursa za kidemokrasia na kuheshimiwa.