1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatakiwa kuwapokea wakimbizi zaidi wa Iraq

Liongo, Aboubakary Jumaa7 Oktoba 2008

Wakati hali ya usalama nchini Iraq ikielezwa kuwa inajaribu kutengamaa taratibu,kwa wakimbizi wa nchi hiyo kurejea nyumbani kwao bado ni hatari.

https://p.dw.com/p/FVF2
Kamishna wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR Antonio Guterres.Picha: picture-alliance/ dpa

Kutokana na hali hiyo, wanaharakati wa haki za binaadamu, pamoja na mashirika yanayohusika na wakimbizi yametoa wito kwa Marekani kufungua mlango zaidi wa kupokewa wakimbizi hao wa Iraq.


Serikali ya Marekani imeweza kutimiza lengo lake ililojiwekea la kuwapokea wakimbizi kutoka Iraq elfu 12 kwa kipindi cha mwaka mmoja kilichomalizika wiki iliyopita, na kuahidi kuongeza idadi hiyo hadi kufikia wakimbizi elfu 17 kipindi kijacho.


Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linasema kuwa kwa wastani kuna wakimbizi wa Iraq kiasi cha millioni moja unusu katika nchi za Syria, Jordan na na nchi nyingine jirani, ambapo elfu 95 kati yao wanatafuta hifadhi ya ukimbizi nchini Marekani.


Hata hivyo pamoja na mashirika ya kutetea haki za binaadamu na yale ya wakimbizi kuipongeza Marekani kwa kutimiza lengo lake hilo, lakini yanasema kuwa kiwango cha wakimbizi waliyoruhusiwa ni kidogo mno.


Kristele Younes kutoka shirika la kimataifa la wakimbizi, anasema kuwa idadi ya wakimbizi elfu 17 ambao Marekani imejiwekea mwaka huu kuwapa hifadhi ni ndogo sana kutokana na wingi wa wakimbizi hao.


Mengi ya makundi ya haki za binaadamu na yale yanayowahudumia wakimbizi yanaona kuwa Marekani inawajibika kwa wakimbizi hao kutokana na kwamba ndiyo iliyoanzisha vita nchini Iraq vilivyopelekea ukimbizi wao.


Mapema mwezi uliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilianisha maendeleo ya mpango wa kuwapa hifadhi wakimbizi wa Iraq pamoja na miradi mbalimbali ya misaada kwa wakimbizi hao.


Mratibu maalum wa Marekani katika suala la wakimbizi wa Iraq, balozi James Foley alisema kuwa  serikali hiyo itawaruhusu maelfu ya wakimbizi kuingia nchini Marekani katika kipindi cha mwaka 2009.


Balozi Foley kwa upande mwengine aliishutumu serikali ya Iraq kwa kushindwa kutoa msaada kulishughulikia suala la wakimbizi wa nchi hiyo.


Amesema kuwa Serikali hiyo haiko makini katika juhudi za kuandaa mipango ya kuwapokea idadi kubwa ya wakimbizi watakaorejeshwa.


Serikali hiyo ya Iraq inashutumiwa kuwa pamoja na kupata kiwango kikubwa cha fedha kinachotokana na mapato ya mafuta lakini imeshindwa kuwahudumia kiasi cha wakimbizi wa ndani millioni nne.

Wafuatiliaji wa mzozo wa wakimbizi wa Iraq pamoja na mashirika ya haki za binaadamu wana wasiwasi juu ya mipango ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao wa Iraq.


Phebe Marr mwandishi wa riwaya  iitwayo The Modern History of Iraq anasema kuwa kuna uzuri na ubaya kwa wakimbizi hao kurudi nyumbani.


Pamoja na kwamba hivi sasa hali ni salama, lakini anasema wakimbizi hao watakaporejea watakabiliwa na matatizo mengine, ambapo wengine watakuta maeneo yao yamechukuliwa na watu wengine, na vile vile tatizo la ajira.


Kwa Michael Kocher  ambaye ni afisa katika shirika la msalaba mwekundu duniani, madhara yatakayowakumba wakimbizi hao watakaporejea ni makubwa zaidi.


Anasema kuwa wananchi wengi wa Iraq kurejea nyumbani ni sawa na kupata hukumu ya kifo, kwani anasema hali ya usalama bado si shwari.


Shirika hilo la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limetoa taarifa likimtaka rais mpya wa Marekani atakayechaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujayo, kutambua kuwa kuna umuhimu maalum wa kuwasaidia wakimbizi wa Iraq kwa kuongeza misaada ya kiutu pamoja na makazi.