Marekani yataka kuurefusha mkataba wa AGOA | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani yataka kuurefusha mkataba wa AGOA

Utawala wa Rais wa Marekani Barrack Obama unajaribu kulishawishi bunge la Marekani kurefusha mpango wa miaka 14 wa kibiashara unaoyawezesha mataifa ya Afrika kuuza bidhaa zake nchini Marekani bila ya kutozwa ushuru

Mwakilishi wa masuala ya kibiashara wa Marekani Michael Froman amesema mkataba wa kutoa fursa za ukuaji wa kibiashara kwa nchi za Afrika wa AGOA ambao unakamilika mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka ujao umezinufaisha nchi za Afrika na kutoa nafasi za ajira 120,000 nchini Marekani.

Matamshi ya Froman yanakuja siku chache kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi karibu zote za Afrika na viongozi wa Marekani mjini Washington utakaodumu kwa siku tatu kuanzia Jumatatu ijayo unaonuia kuimarisha mahusiano kati ya Marekani na bara Afrika katika nyanja mbali mbali.

Mpango wa AGOA kujadiliwa katika mkutano wa kilele

Miongoni mwa masuala makuu ambayo yanatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo utakaowaleta pamoja viongozi hamsini wa Afrika ni mkataba huo wa kibiashara wa AGOA.

Mwakilishi wa masuala ya kibiashara wa Marekani Michael Froman

Mwakilishi wa masuala ya kibiashara wa Marekani Michael Froman

Mpango huo wa AGOA ulioanzishwa mwaka 2000 unaruhusu nchi za Afrika hasa katika kanda ya jangwa la sahara kuingiza katika soko la Marekani bidhaa 7,000 tofauti bila ya kutozwa ushuru na takriban nchi arobaini za Afrika zinafuzu kushiriki katika mpango huo wa kibiashara.

Mkuu wa kamati ndogo ya bunge kuhusu masuala ya biashara Devin Nunes amewaambia waandishi wa habari kuwa bunge la Marekani huenda likaidhinisha kurefushwa kwa mkataba wa AGOA kwa kuharakisha mazungumzo ya kibiashara na kushauriana na mamlaka ya kunadi masuala ya biashara TPA na kuyajadili masuala mengine ya kibiashara ambayo yamewekwa pemebeni.

Afrika na Marekani zote zanufaika

Bidhaa kutoka nchi za kanda ya jangwa la Sahara kuelekea Marekani chini ya AGOA na mipango mingine ya kibiashara ilikuwa ya thamani ya dola bilioni 26.8 mwaka jana huku nyingi ya bidhaa hizo zikiwa ni malighafi za mafuta ya petroli huku ambazo sio za sekta ya mafuta zikiwa za thamani ya dola bilioni 4.9 pekee.

Hata hivyo mpango huo umeshutumiwa kwa kuonekana kuzipendelea nchi fulani zikiwemo Nigeria, Afrika Kusini na Angola.Badhi ya viongozi wa Afrika wamesema nchi zao hazina ujuzi wa kiufundi na miundo mbinu ya kuweza kunufaika na fursa zilizopo. Froman amesema utawala wa Rais Obama unapanga kushughulikia changamoto zilizopo na kutanua nafasi za kunufaika kupitia mpango huo.Wabunge wa Marekani pia wanatarajiwa ufanyiwe mageuzi ili Marekani pia iweze kupenyeza zaidi katika masoko ya kibiashara ya Afrika.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com