1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasisitiza mshikamano na Uturuki

24 Agosti 2016

Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden ameunga mkono hatua ya Uturuki kuingia kijeshi ndani ya Syria, kulipiga vita kundi la Dola la Kiislamu-IS. Biden pia amesema wanashirikiana na Uturuki juu ya kumrejesha Gulen.

https://p.dw.com/p/1Jp5j
Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildirim
Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali YildirimPicha: Reuters/M. Aktas/Prime Minister's Press Office

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden ambaye amefanya ziara nchini Uturuki, akizungumza baada ya kukutana na waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim amesema nchi hiyo haina rafiki yeyote mkubwa kuliko Marekani, na kuunga mkono juhudu ya utawala wa rais Recep Tayyip Erdogan katika kuupiga vita ugaidi.

Amesema, ''Ndio sababu niko hapa bwana waziri mkuu, kwa sababu tutasimama bega kwa bega katika kuwapiga vita wale wanaounia kukwamisha demokrasia yetu, na serikali zetu zilizochaguliwa na wananchi. Tutaendelea kupigana pamoja, dhidi ya ugaidi nchini Syria na Iraq''.

Ingawa serikali mjini Damascus imepinga kuingia kijeshi kwa Uturuki ndani ya eneo lake, waasi kwa upande wao wameikaribisha hatua hiyo. Muungano wa Upinzani wenye makao yake mjini Istanbul umetoa tangazo ukisema operesheni hiyo ni uungaji mkono wa juhudi ambazo tayari wanazifanya.

Uwezekano wa kumrejesha Fethullah Gulen

Mbali na masuala yanayohusu vita vya Syria, ziara ya makamu wa rais wa Marekani pia iliazimia kuukarabati uhusiano kati ya nchi yake na Uturuki, ambao umetiwa doa na kuwepo nchini Marekani kwa Ulamaa wa kituruki Fethullah Gulen, ambaye Uturuki inamtuhumu kupanga jaribio la mapinduzi lililoshindwa la tarehe 15 Julai.

Fethullah Gulen, anayetuhumiwa na Uturuki kupanga jaribio la mapinduzi lililoshindwa
Fethullah Gulen, anayetuhumiwa na Uturuki kupanga jaribio la mapinduzi lililoshindwaPicha: Reuters/C. Mostoller

''Wataalamu wetu wa masuala ya sheria, wanashirikiana na wenzao wa Uturuki hivi sasa, kuandaa ushahidi unaokidhi mahitaji ya sheria zetu, kuhusiana na mkataba wa kurejesheana watuhumiwa, ili kumrejesha Gulen. Na tutaendelea kufanya hivyo, kadri mnavyozidi kutoa maelezo zaidi''. Amesema Biden.

Syria yapinga 'uchokozi' wa Uturuki

Tangazo lililotolewa na wizara ya mambo ya nchi za nje ya Syria imetaka kumalizika haraka kwa kile ilichokiita uchokozi wa Uturuki, unaofanywa katika ardhi ya Syria kwa kutumia vifaru na magari ya kijeshi, kwa kusaidiwa na ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Marekani.

Vifaru vya Uturuki viliingia nchini Syria alfajir ya Jumatano
Vifaru vya Uturuki viliingia nchini Syria alfajir ya JumatanoPicha: picture alliance/AP Photo

''Upande wowote unaotaka kuwapiga vita magaidi kwenye ardhi ya Syria, unapaswa kufanya hivyo kwa ashirikiano na serikali ya Syria na jeshi lake, ambalo limekuwa likiyapiga vita makundi ya kigaidi kwa miaka 5 iliyopita'', limesema tangazo hilo la wizara ya mambo ya nchi za nje, na kuongeza kuwa kuliondoa kundi la IS na katika nafasi yake wakawekwa magaidi wanaoungwa mkono na Uturuki, sio vita dhidi ya ugaidi.

Operesheni ya kijeshi ya Uturuki iliyopachikwa jina la ''Ngao ya Euphrates'' imeanza kabla ya mapambazuko leo, ikitajwa kuwa na lengo la kuwafurusha wapiganaji wa IS kutoka mji wa Jarablus wanaoudhibiti, na pia kulisaka kundi la wanamgambo wa kikurdi lijulikanalo kama PYD.

Mvutano huu mpya kati ya Uturuki na kundi la IS umeibuka baada ya makombora kurushwa ndani ya Uturuki, kutokea mji wa mpakani ndani ya Syria, ambao uko mikononi mwa kundi hilo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, dpae

Mhariri: Mohammed Khelef