1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Viwango vya haki za binadamu vinapungua duniani

John Juma
13 Aprili 2022

Serikali ya Marekani imesema haki za binadamu zinazidi kushuka ulimwenguni kama inavyoshuhudiwa katika vita nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/49tEC
Ukraine Bilderchronik des Krieges | Bucha
Picha: Mykhaylo Palinchak/ZUMA PRESS/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema kwa miaka mingi sasa wameshuhudia viwango vya juu vya kushuka kwa demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu katika pande nyingi za ulimwengu.

Aliyasema hayo alipokuwa akitoa ripoti ya kila mwaka ya wizara yake kuhusu haki za binadamu. 

Blinken ametaja vita vya kikatili vinavyoendelezwa na Urusi nchini Ukraine kama moja ya sababu mbaya zaidi ya kushuka kwa haki za binadamu, huku akivishutumu vikosi vya Urusi kwa unyama ulioenea katika maeneo waliyochukua.

Blinken pia ameishutumu China kwa kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu walio wachache wa Uyghur, na vilevile Taliban kufuatia kamatakamata yake ya kiholela dhidi ya wanawake, waandamanaji na wanahabari.