1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasema itailinda Ukraine dhidi ya Urusi

Zainab Aziz Mhariri: Sekione Kitojo
23 Aprili 2019

Mchekeshaji Volodymyr Zelensky, anayezingatiwa kuwa mwanagenzi wa siasa ameshinda kwa kishindo katika uchaguzi wa rais nchini Ukraine. Jee ataweza kukabiliana na Vladimir Putin wa Urusi?

https://p.dw.com/p/3HGbv
Ukraine, Kiew: Wolodymyr Selenskyj
Picha: picture-alliance/dpa/Stringer

Volodymyr Zelensky sasa ameingia katika ulingo wa siasa nchini Ukraine licha ya kutokuwa na tajiriba ya kisiasa, nchi ambayo ipo mahala pa hatari kubwa ambapo nchi za magharibi zinavutana na Urusi kwa mara nyingine tangu kumalizika vita baridi.

Iwapo kiongozi huyo mpya wa Ukraine ataweza kukabiliana na sungura wa kisiasa Vladimir Putin, mwenye tajiriba kubwa katika mambo ya ujasusi na ambae ameiongoza Urusi kwa miaka takriban 20, ni  jambo  litakaloonekana baadae.

Hata hivyo Zelensky amesema anaazimia kuendelea kuilekeza Ukraine katika upande wa nchi za magharibi. Lakini pia ameahidi kuisogelea Urusi haraka ili kufanya mazungumzo juu ya kuyamaliza mapigano katika jimbo la viwanda la mashariki mwa Ukraine ambako watu wanaotaka kujitenga wanaendesha mapambano dhidi ya Ukraine kwa kuungwa mkono na Urusi. Watu zaidi ya 13,000 wameshauawa kutokana na mgogoro huo ulioanza miaka mitano iliyopita. Swali ni Jee Zelensky ataweza kufanikiwa zaidi kuliko rais wa hapo awali katika juhudi za kukomesha mapigano.

Petro Poroschenko Rais wa Ukraine anayeondoka baada ya kushindwa uchaguzi
Petro Poroschenko Rais wa Ukraine anayeondoka baada ya kushindwa uchaguziPicha: picture-alliance/dpa/Tass/A. Marchenko

Mtaalamu kutoka taasisi ya masuala ya kimataifa ya nchini Finland Arkady Moshes amesema Urusi bila shaka itajaribu kuutumia uanagenzi wa siasa wa Zelensky. Katika uchaguzi uliofanyika jumapili iliyopita Zelensky mwenye umri wa miaka 41 alishinda kwa kuzoa  asilimia 73 ya kura na kumwangusha vibaya Rais aliyekuwamo madarakani Petro  Poroshenko aliyeambulia  asilimia 23 tu ya kura.

Rais huyo anayeondoka Petro Poroshenko jana jioni aliwahutubuia maalfu ya wafuasi wake mjini Kiev na kuwahakikishia kuwa licha ya kushindwa kwenye uchaguzi wa Jumapili hana nia ya kuacha siasa. Marekani imesema iko tayari kushirikiana na rais mpya wa Ukraine na hapo jana Rais Donald Trump alimpongeza Zelenysky kwa ushindi wake. Marekani imesema itashirikiana na kiongozi huyo mpya katika kuilinda Ukraine dhidi ya Urusi.

Pamoja na hatua ambazo Zelenksy amesema atachukua ni kuendeleza juhudi ili mkataba wa Minski utekelezwe. Mkataba huo uliotiwa saini mnamo mwaka wa 2015 ni juu ya kuutatua mgogoro baina ya Ukraine na Urusi na ulifikiwa kutokana na juhudi za kimataifa. Zelensky  pia  amesema ataimarisha juhudi ili Ukraine ijiunge na jumuiya ya kijeshi ya NATO pamoja na Umoja wa Ulaya.

Vyanzo:/AP/AFP