Marekani yaonya kuhusu Yemen na Ugaidi. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 05.01.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Marekani yaonya kuhusu Yemen na Ugaidi.

Marekani imeonya kwamba machafuko yaliyopo nchini Yemen, yanatishia udhabiti wa dunia, hali ambayo pia ilisababisha mataifa ya magharibi kufunga balozi zao katika mji mkuu wa nchi hiyo, Sanaa.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hilary Clinton, aonya kuhusu udhaifu nchini Yemen.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hilary Clinton, aonya kuhusu udhaifu nchini Yemen.

Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kukutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Hamad bin Jassem bin Habr al Thani, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hilary Clinton amesema udhaifu ulioko nchini Yemen ni kitisho kwa eneo hilo na hata pia kwa dunia nzima na kwamba wanafahamu kuwa hiyo ni changamoto kubwa lakini ni lazima kuikabili.

Amefahamisha kwamba Marekani imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Qatar pamoja na washirika wake wengine katika kupambana na tatizo hilo.

Bibi Clinton amesema kumekuwa na mapigano kadhaa nchini Yemen, na yamekuwa yakizidi kuwa mabaya huku watu wengi wakijihusisha nayo, na kwamba sasa ni wakati kwa jumuia ya kimataifa kuweka wazi kwa Yemen kwamba kuna matarajio na masharti juu ya kuendelea kuisaidia serikali.

Yemen yageuka pepo ya wapiganaji: Yemen kwa sasa imekuwa ngome ya makundi ya kigaidi, ambapo pia mtuhimiwa wa jaribio la kulipua ndege ya Marekani wakati wa sikukuu ya Krismas anaelezwa kupata mafunzo yake nchini humo, yaliyotolewa na mtandao wa Al Qaeda.

Blutiger Machtkampf an der jemenitisch-saudischen Grenze

Jeshi la Yemen likikabiliana na wapiganaji waliojificha nchini humo.

Aidha kitisho kilichotolewa na mtandao huo cha kufanya mashambulizi katika mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa, kilisababisha Marekani kuufunga ubalozi wake mjini humo, hatua mabyo ilifuatwa na Uingereza na Ufaransa, huku ubalozi wa Japan ukisimamisha huduma zake.

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nchi za nje wa Marekani ametangaza kwamba ubalozi wa nchi hiyo utafunguliwa leo.

Rais Obama kukutana na wakuu wa vyombo vya Usalama nchini mwake: Wakati huohuo, Rais Barack Obama leo anatarajiwa kutangaza mabadiliko ya kwanza ya orodha ya magaidi ya nchi hiyo, pamoja na matokeo ya awali ya uchunguzi kuhusiana na jaribio la shambulio la kigaidi lililofanywa wakati wa sikuku ya Krismas.

Barack Obama in Cairo

Rais Obama anakutana leo na wakuu wa vyombo vya usalama nchini humo.

Rais wa Marekani atazungumzia mabadiliko hayo kwa mara ya kwanza, mara baada ya mkutano wake wa leo na wakuu wa Shirika la Ujasusi la nchi hiyo pamoja na wakuu wa taasisi za serikali zinazoshughulika na usalama wa taifa.

Mazungumzo hayo yatakayofanyika katika Ikulu ya Marekani yatalenga pia katika uchunguzi unaoendelea kuhusiana na jaribio lililoshindwa la kuilipua ndege ya Marekani, kuimarisha upeanaji taarifa za mfumo wa kuwafuatilia magaidi pamoja na hatua za kuimarisha operesheni za kukabiliana na ugaidi.

Rais Obama pia atapokea taarifa juu ya uchunguzi kutoka kwa Mkurugenzi wa FBI Robert Mueller, atapewa pia taarifa za mashtaka yanayomkabili Umar Farouk Abdulutallab, aliye jaribio kulipua ndege wakati wa krismas, ripoti ambayo itatolewa na Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo Eric Holder.

Viongozi wengine watakaowasilisha ripoti zao ni pamoja na Waziri wa Usalama wa ndani wa nchi hiyo Janet Napolitano, naye mshauri wa Rais Obama katika masuala ya kukabiliana na ugaidi John Brennan ataweka hadharani matokeo ya uchunguzi wake kuhusiana na mfumo wa orodha, ambapo pia wakuu wa taasisi za usalama watazungumzia kuhusiana na mabadiliko ambayo tayari wameyafanya.

Mkutano huo wa Rais Obama na wakuu wa vyombo vya usalama nchini humo, utahudhuriwa pia na Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Robert Gates na Mambo ya Nchi za Nje wa nchi hiyo Hilary Clinton

Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhan

 • Tarehe 05.01.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LLFv
 • Tarehe 05.01.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LLFv
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com