1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yamuunga mkono mbabe wa kivita Libya

Mohammed Khelef
20 Aprili 2019

Rais Donald Trump alizungumza kwa simu na mbabe wa kivita wa Libya, Jenerali Khalifa Haftar, akimuahidi kumuunga mkono, licha ya jitihada za Umoja wa Mataifa kusitisha mapigano ya kuwania udhibiti wa Tripoli. 

https://p.dw.com/p/3H7w7
LNA Chef Khalifa Haftar
Picha: picture-alliance/ Balkis Press

Katika mazungumzo hayo ya jana, Trump na Haftar walijadiliana hatua za kupambana na ugaidi na haja ya kufikia amani na utangamano nchini Libya, kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani. 

Taarifa ya Ikulu hiyo inasema kwamba Trump alilitambuwa jukumu muhimu la Jenerali Haftar katika kupambana na ugaidi na kulinda rasilimali ya mafuta ya Libya. 

Marekani inaungana sasa na Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu katika kumuunga mkono mbabe huyo wa kivita, ambaye mapambano yake ya kutwaa madaraka yanatishia kuirejesha tena Libya kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Ikulu ya Marekani haikusema kwa nini ilichelewa kutoa taarifa ya mazungumzo hayo ya simu kati ya Trump na Haftar, lakini wachunguzi wanasema uamuzi wa Trump kumsifia Haftar ni ushahidi wa kwa nini jenerali huyo muasi amekuwa na dhamira ya kuutwaa mji mkuu, Tripoli, unaodhibitiwa na serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, anayetambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Kamanda huyo wa kijeshi anaunga mkono serikali hasimu ya Libya yenye makaazi yake mashariki mwa nchi hiyo na amekataa kuyatambua mamlaka ya serikali iliyo mjini Tripoli.

Nguvu za Haftar kimataifa

Auseinandersetzungen zwischen Haftars Streitkräften und der libyschen Regierung in Tripolis
Vikosi vya serikali vikipigana na waasi wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar.Picha: picture-alliance/AA/H. Turkia

Siku ya Alhamis (Aprili 18), Urusi na Marekani zilipinga rasimu ya azimio la Uingereza ambalo lilikuwa likiungwa mkono na Ufaransa na Ujerumani kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka usitishwaji mapigano nchini Libya.

Urusi ilisisitiza kutokuwepo ukosowaji wowote dhidi ya Haftar kwenye rasimu ya azimio hilo, huku Marekani ikitaka ipewe muda zaid kufikiria hali ilivyo.

Wanadiplomasia wanasema ishara kutoka Washington inakwenda mbali zaidi katika kuelezea mkakati wa kichokozi wa Haftar licha ya ukosoaji mkubwa kutoka mataifa ya Ulaya na Umoja wa Mataifa.

"Haftar anaamini anapaswa kupambana hadi mwisho," alisema mwanadiplomasia mmoja wa Umoja wa Mataifa kwam masharti ya kutotajwa jina.

Licha ya kurejeshwa nyuma kijeshi, Haftar anashikilia kwamba anaweza kushinda, kwa mujibu wa wanadiplomasia wengine wengi.

Taarifa za mazungumzo yake ya simu na Trump "zinaweka wazi" nafasi ya Marekani, alisema mwanadiplomasia mwengine, baada ya Uingereza kupambana kwa siku tano bila mafanikio ya kupitisha azimio la usitishwaji mapigano na kutoa fursa ya kuwafikia raia waliokwama kwenye maeneo ya mapambano.

Nguvu ya Sarraj kimataifa

Libyen - Premier Fajis al-Sarradsch
Waziri Mkuu wa Libya Fayez al-SarrajPicha: Getty Images/AFP/F. Belaid

Kimataifa,  Waziri Mkuu Sarraj, ambaye udhibiti wake wa nchi ni dhaifu sana, anaungwa mkono na Qatar na Uturuki tu.

Ni wazi kwamba Haftar asingelianzisha operesheni ya kuutwaa mji mkuu, Tripoli, kama hakupewa ruhusa na waungaji mkono wake, na sasa kumfanya arejee chini kunategemea na waungaji mkono hao, walisema wanadiplomasia.

Matokeo yoyote yale ya azimio la Uingereza, namna mchezo wa kidiplomasia ulivyofikia kuhusiana na suala la Libya umeyashusha hadhi madaraka ya Umoja wa Mataifa.

Kuanza kwa operesheni ya Haftar kuelekea Tripoli kulisadifiana na ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, nchini Libya aliyekuwa akishinikiza kuitishwa kongamano la maridhiano ya kitaifa.

Kongamano lilifutwa ghafla na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa Libya, Ghassan Salame, ambaye wiki hii aliita operesheni hiyo ya Haftar kuwa ni mapinduzi ya kijeshi. 

Ikiwa Haftar atafanikiwa kuchukuwa madaraka, heshima ya Salame na Umoja wa Mataifa zitakuwa mashakani.

AP/Reuters