1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yamshutumu Kagame

Admin.WagnerD4 Januari 2016

Marekani imeelezea kukatishwa tamaa na uamuzi wa Rais Paul Kagame wa Rwanda kuwania muhula wa tatu madarakani na kupuuza misingi ya demokrasia.

https://p.dw.com/p/1HXaA
Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Rais Paul Kagame wa Rwanda.Picha: picture-alliance/dpa/G. Ehrenzeller

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani John Kirby amesema katika taarifa Rais Paul Kagame anapuuza fursa ya kidemokrasia ya kuimarisha asasi za kidemokrasia ambazo wananchi wa Rwanda wamepigania kwa miaka 20 kuzianzisha.

Kagame ambaye aliwahi kuwa kipenzi cha mataifa ya Magharibi amesema Ijumaa iliopita atawania tena urais kwa mujibu wa marekebisho ya katiba ambayo yameungwa mkono kwa sauti moja na wananchi.

Wapiga kura waliunga mkono kwa wingi marekebisho ya katiba yenye kumruhusu Kagame mwenye umri wa miaka 58 kuwania muhula mahsusi wa tatu katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka 2017.

Shutuma hizo za Marekani zinakuja wakati nchi hiyo ikizidi kuwa na wasi kwa kuongezeka kwa idadi ya viongozi wa Kiafrika wanaon'gan'gania madaraka.Marekani na Umoja wa Ulaya zimekuwa zikielezea wasi wasi wao mkubwa juu ya hatua hiyo.

Kuheshimu katiba

Marekani inaamini kukabidhiana madaraka kwa mujibu wa katiba ni muhimu kwa ajili ya kuwepo kwa demokrasia madhubuti na kwamba juhudi zinazofanywa na viongozi walioko madarakani ku'gan'gania madaraka zinadhoofisha asasi za kidemokrasia.

Msemaji wa wizara ya Mambo ya nje ya Marekani John Kirby.
Msemaji wa wizara ya Mambo ya nje ya Marekani John Kirby.Picha: picture alliance/AA/S. Corum

Wakati Rwanda ikielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu,uchaguzi wa rais mwaka ujao na uchaguzi wa bunge mwaka 2018 Marekani imeitaka Rwanda kuhakikisha na kuheshimu haki za raia wake kutumia uhuru wao wa kujieleza, kufuata itikadi waitakayo na kukusanyika kwa amani ambazo ni alama za demokrasia.

Mashirika ya haki za binaadamu yanakiri kwamba Kagame anaungwa mkono kwa sauti kubwa nchini Rwanda lakini yanaishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kunyamazisha vyombo vya habari na sauti za upinzani madai ambayo serikali inayakanusha.

Kagame aidhibiti Rwanda

Kagame ambaye amekuwa rais tokea mwaka 2000 amekuwa akiidhibiti nchi hiyo kikamilifu tokea kikosi chake cha waasi kilipoingia Kigali kukomesha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Alikuwa akiruhusiwa kutawala kwa mihula miwili lakini Rwanda imeidhinisha mabadiliko ya katiba mwaka jana ambayo yatamuwezesha kubakia mabadarakani hadi mwaka 2034 iwapo atashinda katika uchaguzi.

Wananchi wa Rwanda wakati wa kura ya maoni juu ya marekebisho ya katiba.
Wananchi wa Rwanda wakati wa kura ya maoni juu ya marekebisho ya katiba.Picha: picture-alliance/dpa/J. Johannsen

Marekani ni mfadhili mkuu kwa Rwanda na inaipatia nchi hiyo msaada wa kijeshi.Kwa muda mrefu imekuwa ikimpongeza kwa kulifanyia mageuzi taifa hilo tokea mauaji ya kimbari.

Nchi jirani ya Burundi ambayo ina historia kama ya Rwanda ya mapigano ya kikabila ilitumbukia katika machafuko kutokana na tangazo la Rais Piere Nkurunziza kwamba atawania muhula wa tatu jambo ambalo limeshutumiwa na upinzani kuwa linakiuka katiba.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef