1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yalegeza vikwazo kuruhusu misaada kwenda Somalia

Aboubakary Jumaa Liongo3 Agosti 2011

Serikali ya Marekani imetangaza kulegeza baadhi ya vikwazo vyake kwa kuruhusu mashirika ya misaada kupeleka misaada hiyo kwenye maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Al Shabaab

https://p.dw.com/p/129sp
Misaada ikishushwa MogadishuPicha: dapd

Hatua hiyo ina maana kuwa mashirika ya kujitolea hayatokabiliwa na hatua za kisheria dhidi yao kwa kupeleka misaada kwenye maeneo hayo. Hata hivyo vikwazo dhidi ya wale wanaojiita wababe wa vita vinaendelea kubakia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Mark Toner amesema nchi yake kuanzia sasa itayapatia vibali na kandarasi mashirika hayo ya kujitolea hata kama kwa bahati mbaya misaada hiyo itaangukia katika mikono ya wanamgambo wa Al Shaabab.

Wanamgambo wa Al Shaabab wanadhibiti eneo kubwa la kusini na katikati mwa Somalia maeneo ambayo ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na ukame uliyosababisha njaa.

Mwaka 2008 Marekani ililiwekea vikwazo kundi hilo la Al Shaabab na kutangaza kuwa ni kosa la uhaini kwa yoyote atakayelipatia msaada wowote kundi hilo. Marekani imesema vikwazo hivyo vya mwaka 2008 havina nia ya kuathiri shughuli za makundi ya misaada.

Mapema Mratibu wa kitengo cha misaada ya dharura cha Umoja wa Mataifa bibi Valarie Amos alionya juu ya kitisho cha wanamgambo hao wa Al Shabaab kuathiri usambazaji wa misaada.

"Bila shaka tuko tayari kuzidisha misaada yetu kwa kiwango kikubwa kwani uwezo huo tunao, lakini pia tunakabiliwa na makundi ya wanamgambo ambao wanasema hawatutaki kuwepo huko hata hivyo tunafanya kila tuwezalo kupitia majadiliano nao ili kubadilisha hali hiyo."

Naye msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney amesema nchi hiyo ambayo imechangia zaidi ya dola millioni 450 kwa ajili ya misaada katika pembe ya Afrika mwaka huu wa fedha, imedhamiria kwa dhati kuwasaidia watu wa Somalia.

Kundi la Al Shabaab liliyatimua mashirika ya misaada miaka miwili iliyopita likiyatuhumu kuwa yalikuwa yakifanya ujasusi kwa niaba ya mataifa ya magharibi.

Mashirika hayo ya misaada ya kibinaadamu yamesema kuwa ukame uliyolikumba eneo eneo la pembe ya Afrika haujawahi kutokea katika kipindi cha miongo sita.

Mapema Rais, Sharif Sheikh Ahmed wa serikali ya mpito nchini Somalia akiwa ziarani nchini Sudan alilalamika juu ya misaada michache kutoka mataifa ya Kiarabu na yale ya Kiafrika.

Kiongozi alikuwa Sudan kuomba msaada ikiwa ni wiki moja kabla ya kuitishwa mkutano wa wafadhili kwa ajili ya watu walioathirika na ukame huko Somalia.

Mjini Berlin Waziri wa Misaada ya Maendeleo wa Ujerumani, Dick Niebel amekitaka kikosi cha kulinda amani cha Afrika huko Somalia AMISON, kuhakikisha kunakuwepo na usalama katika kiwanja cha ndege mjini Mogadishu, kwa ajili ya ndege za misaada ya chakula.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/ZPR

Mhariri:Josephat Charo