Marekani yalaumiwa na nchi za Afrika,Brazil na WTO kuhusu suala la ruzuku kwa wakulima wa Pamba | Masuala ya Jamii | DW | 24.03.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Marekani yalaumiwa na nchi za Afrika,Brazil na WTO kuhusu suala la ruzuku kwa wakulima wa Pamba

Wakulima wa pamba barani Afrika hawafaidiki kilimo hicho

default

Francois Traore, Rais wa chama cha wakulima wa pamba barani Afrika

Nchi zinazolima pamba  barani Afrika zinataraji kwamba hatua iliyopangwa kuchukuliwa na Brazil ya kulipiza kisasi dhidi ya Marekani katika vita vya kibiashara  baada ya kufanikiwa kupewa idhini ya kuchukua hatua hiyo na bodi inayohusika kutatua mivutano katika shirika la biashara duniani WTO  italeta pia mafanikio upande wao  ingawa nchi hizo  zinaonekana kuwa kimya kuhusu suala la kuchukua hatua kama ya Brazil dhidi ya Marekani kuhusiana na kuendelea kutumia  ruzuku katika uzalishaji wa pamba.

Burkina faso ikiwakilishwa na mjumbe wake Prosper Vokouma katika Umoja wa mataifa mjini Brussels na ambaye pia ni mratibu wa kundi la C4  inasema kwamba hawafaidiki moja kwa moja na Uamuzi wa shirika la WTO.Kundi la C4 linajumuisha nchi nne za Afrika  ambazo zinasafirisha kwa wingi Pamba  ambazo ni Benin,Burkina Faso,Mali na Chad.Nchi hizo zimefanikiwa kulipeleka suala la Pamba katika shirika la biashara duniani la WTO.

Vokouma anasema kwamba Uamuzi uliopitishwa na WTO  unaotoa uhalali  katika mapendekezo ya nchi za kundi la C4.Ansema kwamba Uamuzi huo umekosoa vikali  pamoja na kupinga suala la ruzuku. Bodi ya kutatua mivutano ya shirika la biashara duniani la WTO imethibitisha kwamba hatua ya Marekani yakuendelea kutumia ruzuku inawaharibia wakulima wa nchi zingine  kwasababu ya athari zake  katika suala la bei kwenye masoko.

Marekani haipendezwi na hatua ya kunyooshewa kidole cha lawama kuhusiana na suala hilo.Kiasi cha wakulima wakubwa 2500 nchini Marekani wanagawana miongoni mwao zaidi ya dollar billioni 3 kila mwaka ambapo wakulima millioni 20 hadi 30 wa zao la Pamba barani Afrika wanaishi katika maisha ya tabu na kusikitisha  kwasababu hawafaidiki na chochote kutokana na juhudi zao za ukulima wa pamba  na mwisho hawawezi hata kukimu mahitaji yao ya chakula cha kila siku.

''Tunalazimika  hapa kuzishughulikia familia kubwa na ndio sababu tunalima pamba.Ukulima huo unapasa kutuletea kiasi cha kutosha cha fedha.Lakini kutokana na mashindaano yasiokuwa ya haki hatufaidiki na chochote.''

Brandrodung in Brasilien Urwald Ackerland

Wakulima wa pamba Afrika wanaililia Marekani ikomeshe mipango yake ya kutoa ruzuku kwa wakulima wake

 Uchunguzi uliofanywa na mashirika kadhaa ya kimataifa unaonyesha kwamba ikiwa Marekani itaacha kabisa kutumia ruzuku basi bila shaka bei ya zao la pamba duniani itaongezeka  kwa asilimia 14.Kwa mujibu wa shirika la msaada la Oxfam hatua kama hiyo itachangia kuongeza pato  ambalo linaweza kuwalisha watoto millioni   moja zaidi kwa mwaka au hata kulipia karo za shule za watoto millioni mbili katika eneo la Afrika Magharibi.

''Kuna kundi kubwa la washawishi nchini Marekani linalowatetea wakulima wa pamba,ambalo linamafungamano mazuri na bunge la nchi hiyo,hali hiyo ndiyo inayozuia  kufanyika mageuzi.Serikali ya Marekani ikitaka kufanya mageuzi inapata upinzani kutoka bungeni''

Vokouma kutoka Burkina Faso anasema ikiwa Brazil itafanikiwa kuitia kishindo Marekani kukomesha hatua yake ya kutumia ruzuku kwa ajili ya  wakulima wake  pia itazisaidia kupata ushindi  japo sio wa moja kwa moja nchi za kundi la C4 pamoja na nchi zingine 32 zinazozalisha Pamba barani Afrika na hata  kuinua uaminifu wa shirika la WTO.

Sauti za kundi la C4 zinasikika baada ya Brazil mnamo tarehe 8 mwezi wa Marchi  kuchapisha orodha ya bidhaa 100 za Marekani ambazo itaziongezea kiwango cha ushuru kufikia thamani ya dolla millioni 591.Bidhaa hizo ni pamoja na matairi,magari.vipodozi,bidhaa za chakula,dawa na pamba.

Aidha Brazil pia ilitangaza baadaye orodha zaidi ya vitu kutoka Marekani ambavyo itavitoza ushuru ikiwemo nakala za kanda za Muziki,vitabu na hata mikanda ya Cinema.Brazil imetoa muda wa mwisho wa siku 20  wa kufanyika mazungumzuo kuhusiana na vikwazo hivyo.Hatua hiyo ya Brazil imechukuliwa baada ya jopo maalum la shirika la bishara duniani la WTO kupitisha uamuzi wa kihistoria  kuhusiana na vita vya kibiashara kati ya Brazil na Marekani ambapo iliidhinisha Brazil kuchukua hatua inayotaka dhidi ya Marekani kutokana na mipango yake ya kuuza vitu kwa bei rahisi kupita kiasi kinyume na ilivyokubaliana na Brazil.

Mwandishi: Kriesch Adrian ZR/Saumu Mwasimba

Mhariri AbdulRahman.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com