1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yajiondoa rasmi kwenye mkataba wa INF

Amina Mjahid
2 Agosti 2019

Marekani inajiondoa kwenye makubaliano ya kupunguza silaha za masafa ya kati ambayo yalizitaka Marekani na Muungano wa Kisovieti kupunguza kabisa makombora ya ardhini yanayoweza kurushwa kufikia kilomita 500 hadi 5,500.

https://p.dw.com/p/3NEMq
USA Mike Pompeo Aufkündigung INF-Vertrag
Picha: Getty Images/C. Somodevilla

Kwa mara ya kwanza; mataifa hayo mawili yaliyo na nguvu duniani yalikubaliana kuondoa aina zote za silaha za nyuklia na pia kusaini uchunguzi wa vinu vyao vya nyuklia kuhakikiSa pande zote mbili zinatekeleza makubaliano hayo.

Chini ya miaka mitano baada ya makubaliano hayo kusainiwa, makombora 2,692 yaliharibiwa. 

Hatua hii ilikuwa muhimu sana kwa Ujerumani iliyoshuhudia maandamano makubwa katika miaka ya '70 na '80 dhidi ya kuwekwa silaha za nyuklia.

Lakini upinzani huo hakufanikiwa, kwani zaidi ya makombora 100 aina ya Pershing yalikuwepo magharibi mwa Ujerumani. 

Kuanzia mwaka 2014, Marekani na Urusi zimekuwa zikikwaruzana na kulaumiana mara kwa mara kuyavunja makubaliano hayo.

Makombora aina ya 9M729 ya Urusi ndio yaliyoleta mvutano mkubwa.

Urusi inasema makombora hayo yanaweza kufikia umbali wa chini ya kilomita 500 inayokubalika katika makubaliano hayo ya INF, jambo ambalo Marekani inakanusha vikali. 

Putin amfuata Trump kujiondoa INF

Infografik INF-Vertrag EN

Mwezi Februari mwaka huu, Rais Donald Trump wa Marekani alianzisha mpango wa kuiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya kupunguza silaha za masafa ya kati ya kinyuklia (INF) na muda mfupi baadaye Rais Vladimir Putin wa Urusi naye akatangaza kufanya vivyo hivyo. 

Kwa takriban miezi sita iliyopita wanadiplomasia wa Ujerumani na Ufaransa wamekuwa wakijizatiti kuuokoa mkataba huo, kwa mujibu wa Fabrice Pothier, mshauri mkuu katika taasisi ya kimataifa ya masuala ya kimkakati na aliyewahi kuwa mkuu wa sera katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Kwa upande wake, Ulrich Kühn kutoka Taasisi ya Utafiti wa Amani na Sera za Usalama katika Chuo Kikuu cha Hamburg nchini Ujerumani amesema kuvunjika kwa makubaliano ya INF ni habari mbaya sana kwa usalama wa bara la Ulaya, kwani hatua hiyo itamaanisha bara hilo linarejea nyuma katika historia ya miaka ya 80.

"Tutashuhudia kwa mara yengine tena makombora ya Urusi yakilenga mataifa ya Magharibi," alisema Kühn alipozungumza na DW na kuongeza kuwa "huenda kwa mwaka mmoja au miwili makombora ya Magharibi yakailenga Urusi."

Afisa wa zamani wa NATO, Fabrice Pothier, ameitolea wito Ufaransa na Ujerumani kuendelea na juhudi zao za kidiplomasia na kujaribu kuwa na mazungumzo na Urusi, akisema Urusi kwa sasa inapaswa kujizuwia kuweka makombora ya masafa ya kati magharibi mwa milima ya Ural.