Marekani yaitaka Urusi kushinikizwa zaidi kuhusu mzozo wa Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Marekani yaitaka Urusi kushinikizwa zaidi kuhusu mzozo wa Ukraine

Marekani imeliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa kuna haja ya kuishinikiza zaidi Urusi ili iheshimu makubaliano ya kusitsisha mapigano nchini Ukraine huku Urusi ikikanusha ni kitisho kwa jirani yake Ukraine

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lenye nchi wanachama 15 lilfanya kikako cha 26 cha dharura hapo jana kuhusu mzozo wa Ukraine.Makubaliano ya kusitisha mapigano katika eneo la mashariki mwa Ukraine kati ya waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo hilo na serikali yaliyofikiwa mnamo tarehe tano mwezi Septemba mjini Minsk yamekiukwa na nchi za magharibi zinahofia kuwa vita kamili huenda vikatokea hivi karibuni.

Ukraine imesema inawatuma wanajeshi zaidi katika eneo hilo la mashariki kwasababu ina hofu waasi wanaoungwa mkono na Urusi wataanzisha mashambulizi mapya licha ya Urusi kukanusha kuwa imetuma zana za kijeshi kuwahami waasi hao.

Jumuiya ya kimataifa ichukue hatua zaidi

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kile kinachohitajika ni kuongeza mbinyo dhidi ya Urusi hadi pale itapoyaheshimu makubaliano ya Minsk na kuchagua njia ya kupunguza mzozo huo wa mashariki mwa Ukraine.

Balozi wa Marekani katika umoja wa Mataifa Samantha Power

Balozi wa Marekani katika umoja wa Mataifa Samantha Power

Marekani na Umoja wa Ulaya imeiwekea Urusi vikwazo chungu nzima vya kiuchumi katika juhudi za kuishurutisha kuumaliza mzozo wa Ukraine lakini uasi umeeendelea kupamba moto mashariki mwa Ukraine tangu mwezi Machi mwaka huu.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana mjini Brussels,Ubelgiji Jumatatu wiki ijayo kuijadili hali hiyo lakini haitarajiwi kama watatangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi.

Nato yadai Urusi inaingiza silaha Ukraine

Jumuiya ya kujihami ya NATO imesema imeshuhudia wanajeshi na zana nzito za kijeshi zikiwasili mashariki mwa Ukraine kutoka Urusi.Naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Alexender Pankin amesema madai ya NATO hayaelezei hali halisi ilivyo katika eneo hilo na ni matamshi matupu yaliyojaa uongo wa kuendeleza propaganda.

Kamanda wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Philip Breedlove

Kamanda wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Philip Breedlove

Shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE mapema wiki hii pia liliripoti wachunguzi wake walioko Ukraine wameshuhudia magari ya kijeshi na silaha nzito zikisafirishwa hadi maeneo yanayodhibitiwa na waasi.

Naibu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kisiasa Jeny Anders Toyberg Frandzen amesema umoja wa Mataifa unatiwa wasiwasi mkubwa na uwezakano huo wa kuzuka vita vikubwa Ukraine.

Waziri mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk ametoa hakikisho kuwa nchi yake inafanya kila iwezalo kuupunguza mzozo huo na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov amesisitiza azma ya taifa lake ni kuona suluhisho linafikiwa kwa njia ya mazungumzo ya moja kati ya serikali ya Ukraine na waasi hao.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/dpa

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com