1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka Kongo kuheshimu haki ya kuandamana

Saleh Mwanamilongo
25 Mei 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesisitiza haki ya watu wa Kongo kuandamana kwa amani ili kueleza wasiwasi na matarajio yao.

https://p.dw.com/p/4Rnso
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken azungumza kwa simu na Rais wa Kongo Felix Tshisekedi
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken azungumza kwa simu na Rais wa Kongo Felix TshisekediPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Katika mazungumzo ya simu na Rais Felix Tshisekedi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisisitiza haki ya watu wa Kongo kuandamana kwa amani ili kueleza wasiwasi na matarajio yao. Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema Blinken alisisitiza pia juhudi za Marekani kusaidia uchaguzi huru na wa haki nchini Kongo.

Siku ya Jumamosi, vikosi vya usalama viliwapiga watu kadhaa ikiwa ni pamoja na angalau mtoto mdogo wakati upinzani ulijaribu kuandaa maandamano katika mji mkuu, Kinshasa. Polisi baadaye walisema kwamba waandamanaji walikuwa wamepuuza ratiba ya safari iliyoidhinishwa awali ya maandamano hayo.

Changamoto za kiusalama

Kwenye mazungumzo yake na Tshisekedi ,waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Blinken pia alielezea wasiwasi wake kuhusu kuzuka upya kwa ghasia mashariki mwa Kongo na aliunga mkono tena madai kwamba nchi jirani ya Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23.

Blinken na Tshisekedi walijadili umuhimu na uharaka wa M23 kujiondoa kwenye maeneo wanayoyakalia na kuwapokonya silaha wapiganaji hao kulingana na makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana nchini Angola.

Kwa upande wake Jumanne, Umoja wa Mataifa Umoja pia ulilaani matumizi ya nguvu ya polisi dhidi ya waandamaji mjini Kinshasa siku ya Jumamosi.

''Ukandamizaji wa kikatili''

Polisi walitumia nguvu kuzima maandamano ya upinzani mjini Kinshasa ,juma mosi ya tarehe 20.05.2023
Polisi walitumia nguvu kuzima maandamano ya upinzani mjini Kinshasa ,juma mosi ya tarehe 20.05.2023Picha: JUSTIN MAKANGARA/REUTERS

Miezi saba kabla ya uchaguzi wa rais ambao unatarajiwa kuwa na mvutano mkali, Umoja wa Ulaya na Uingereza pia zililaani matumizi ya nguvu ya polisi dhidi ya waandamaanji wa Kinshasa. Katika taarifa yake, Baraza la Maaskofu wa Kongo,Cenco, lililaani kile lilichoelezea kuwa ni ukandamizaji wa kikatili ambao polisi waliwafanyia waandamanaji.

Akizuru majeruhi wa maandamano hayo waliolazwa hospitalini, siku ya jumatatu, Rais Felix Tshisekedi alipongeza kile alichoelezea kuwa ni ujasiri wa polisi dhidi ya wahuni.

Upinzani umeitisha maandamano mapya hii leo jijini Kinshasa,mbele ya makao makuu ya Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi,CENI. Polisi tayari imeonya kuwa maandamano hayo hayakuruhusiwa na yatazimwa. Maandamano hayo yameitishwa na vyama vya wagombea wanne ambao ni Martin Fayulu, Moise Katumbi, Matata Ponyo na Delly Sesanga.

Uchaguzi wa Desemba 2023

Mbali ya suala la uchaguzi, waandamanaji wamekasirishwa  na kupanda kwa gharama za maisha pamoja na ukosefu wa usalama wa muda mrefu katika eneo la mashariki mwa taifa hilo.

Uchaguzi wa urais umepangwa kufanyika Desemba 20 na Félix Tshisekedi, aliye madarakani tangu 2019, ameonyesha niya ya kuwania muhula wa pili.