1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka China kuwa wazi zaidi

Kabogo Grace Patricia17 Desemba 2009

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton.

https://p.dw.com/p/L6YH
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton.Picha: AP

Marekani imeitaka China kuwa wazi zaidi kuhusu lengo lake la upunguzaji wa gesi zinazoharibu mazingira, huku matumaini ya kufikiwa makubaliano katika mazungumzo ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa yanayoendelea mjini Copenhagen, yakiwa yanazidi kufifia baada ya mwenyeji wa mkutano huo, Denmark kuachana na juhudi za kuandaa waraka wa kupendekeza ufumbuzi wa mzozo uliojitokeza ili kurahisisha majadiliano kufuatia upinzani mkali wa kundi la nchi zinazoendelea, G-77. Kauli hiyo ya Marekani imetolewa na Waziri wake wa Mambo ya Nchi za Nje, Hillary Clinton ambaye yuko mjini Copenhgagen siku moja kabla ya Rais Barack Obama kuwasili katika mkutano huo hapo kesho. Bibi Clinton amesema kuwa mataifa yote tajiri yameahidi kuwa wawazi na kwamba bila ya kuwepo uwazi, makubaliano miongoni mwao yatakuwa yamevunjika.

Wanadiplomasia kutoka duniani kote wanasema kuwa makubaliano kati ya China na Marekani ambapo zote zinatakiwa kupunguza matumizi ya gesi zinazochafua mazingira kwa asilimia 40, yatakuwa muhimu kwa mkataba wowote ule. Bibi Clinton ameongeza kuwa wakati Marekani inajiandaa kushirikiana na nchi nyingine kuhamasisha utoaji wa dola bilioni 100 kwa ajili ya nchi masikini ifikapo mwaka 2020, ushiriki wa nchi yake utategemea mafanikio yatokanayo na mkutano wa Copenhagen.Kiasi cha fedha ambacho nchi tajiri wanatakiwa wakitoe kwa nchi mataifa yanayoendelea ili kukabiliana na ongezeko la ujoto duniani na kuounguza matumizi ya gesi zinazoharibu mazingira, ni moja kati ya masuala muhimu katika mkutano huo wa Copenhagen.

Denmark yaachana na mpango wake

Aidha Waziri Mkuu wa Denmark, Lars Rasmussen amethibitisha hatua ya kuachana na mpango wa kuandaa waraka wa kufikiwa makubaliano ya majadiliano ya hali ya hewa, baada ya kukutana na kundi la G-77, China na makundi mengine. Mkuu wa kundi la G-77 amekanusha shutuma kuwa kundi hilo ndilo kikwazo katika majadiliano hayo, na kuongeza kuwa mazungumzo hayo yanakwama kutokana na kukosekana kwa uwazi. Kwa upande wake, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel akizungumza kutoka Berlin kabla ya kuelekea katika mkutano huo, amesema kuwa taarifa zinazotolewa Copenhagen si nzuri na haziridhishi. Bibi Merkel amesema kuwa mkutano wa Copenhagen utashindikana kama mataifa yote hayatapunguza ongezeko la ujoto duniani kwa nyuzi mbili za ujoto ikilinganishwa na viwango vya zamani.

Kauli ya Umoja wa Ulaya

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umeelezea wasi wasi wake kutokana na maendeleo ya mazungumzo ya hali ya hewa huko Copenhagen, na kutoa mwito kwa pande zinazohusika kuondoa tofauti zao hara ili waweze kufikia mkataba wa hali ya hewa. Katika taarifa yao ya pamoja, mwenyekiti wa sasa wa umoja huo, Sweden na Kamisheni ya umoja huo, imeeleza kuwa Umoja wa Ulaya umetoa mapendekezo muhimu na kuendelea na msimamo wake wa ahadi ya kufanya zaidi, kama wengine hasa mataifa yanayoharibi zaidi mazingira watatekeleza ahadi zao pia. Mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya tayari yameahidi kupunguza matumizi ya gesi zinazoharibu mazingira kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020, kutoka katika viwango vya zamani vya mwaka 1990.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/DPAE)

Mhariri:Abdul-Rahman