Marekani yaitaka China ipunguze utoaji gesi inayoharibu mazingira | Masuala ya Jamii | DW | 05.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Marekani yaitaka China ipunguze utoaji gesi inayoharibu mazingira

Wakati dunia ikijiandaa kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa wa hali ya hewa baadaye mwezi ujao huko Copenhagen Denmark, Marekani imetoa msimamo wake kuhusiana na upunguzaji wa gesi inayoharibu mazingira.

default

Marekani imesema haiko tayari kufikia ,malengo ya upunguzaji wa utoaji wa gesi inayoharibu mazingira mpaka nchi zinazoendelea hususan China itakapofanya hivyo.

Akizungumza mjini Washington, mjumbe wa maalum wa Marekani wa masuala ya hali ya hewa, Todd Stern amesema hakuna nchi yoyote duniani ambayo imebeba majaaliwa ya duniani zaidi ya China.

Ameambia kamati ya bunge la Marekani ya masuala ya nje, kuwa sheria mpya za hali ya hewa zinaweza kujumuisha msamaha fulani kwa baadhi ya mataifa yanayoendelea, ili kuyahakikishia kuwa ukuaji wake wa uchumi auathiriki na sheria hizo, lakini akasema mataifa kama China, India na Brazil ni lazima yapunguze kasi yake ya utoaji wa gesi inayoharibu mazingira unaotokana na kukua haraka kwa uchumi wake.

Matamshi yake hayo yamekuja mnamo wakati kuna mgawanyiko kati ya nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea, hali inayotishia kufikiwa kwa makubaliano ya mkataba mpya wa mabadiliko ya hali hewa katika mkutano wa Copenhagen kuchukua nafasi ya ule wa Kyoto.

Mjumbe huyo maalum wa Marekani wa hali ya hewa, amesema kuna masuala mengi yanayotakiwa kufanyiwa kazi kabla ya mkutano huo wa Copenhagen, na kuonya kuwa maendeleo yamekuwa yakipigwa kwa mwendo wa taratibu mno hususan katika muundo wa majadiliano yatakavyokuwa.

Mwanzoni mwa wiki hii akiwa ziarani nchini Marekani Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliitaka Marekani na Ulaya kuwa mstari wa mbele katika kufikiwa kwa mkataba mpya wa hali hewa huko Copenhagen. Akasema hatua hiyo itayahamasisha mataifa yanayoendelea kutia saini mkataba huo.

Angela Merkel spricht vor dem Amerikanischen Kongress

Kansela Angela Merkel akihutubia bunge Congress, Marekani

´´Iwapo sisi Ulaya na Marekani tutakuwa tayari kukukabaliana na rasimu ya mkataba mpya, basi pia tutazishawishi India na China.´´

Tayari mawaziri kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya wamekwishaanza majadiliano ya jinsi ya kufikia makubaliano ya matumizi ya nishati isiyoharibu mazingira.

Kwa upande mwengine,bunge la Congress linajadili muswaada wa kupunguza utoaji wa gesi inayoharibu mazingira nchini Marekani, muswaada ambao unaoenakana kuwa muhimu sana kwa kufikiwa kwa mkataba mpya mjini Copenhagen.

Katika Bunge la seneti kundi la maseneta wanaharakati wa mazingira limekuwa na vikao na maafisa wa Ikulu ya Marekani kuandaa mapendekezo ambayo yataweza kuungwa mkono kama si mwaka huu, basi mwakani.

Seneta John Kerry kutoka chama cha Rais Obama cha Demokratik amesema juhudi zao ni kujaribu kuweka misingi ambayo muswada huo utaweza kuungwa mkono na kupitishwa.

Seneta Kerry anashirikiana na Lindsey Graham kutoka Republican pamoja na seneta binasi Joseph Lieberman, katika harakati hizo.

Kwa upande mwengine wakati Marekani ikitoa msimamo huo, mkutano wa hali ya hewa unaofanyika huko Barcelona Uhispania kabla ya ule wa Copenhagen, uliendelea tena, baada ya wajumbe kutoka Afrika kuvisusia vikao vya majadiliano.

Wajumbe hao kutoka nchi 50 za Afrika, waliyashutumu mataifa tajiri kwa kushindwa kutimiza ahadi yalizotoa ya kuzuia utoaji wa gesi inayochangia ongezeko la ujoto duniani kwa kiwango cha asilimia 40 ifikapo mwaka 2020 kuanzia mwaka 1990.

Maafisa wanaosimamia majadliano katika mkutano huo wa Barcelona, wamekiri kuwa nafasi ya matumaini ya kuweza kufikiwa kwa mkataba mpya mwezi ujayo, imetoweka.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com