1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaipunguzia Aghanistan dola bilioni 1 za msaada

Rashid Chilumba24 Machi 2020

Marekani imesema inaondoa msaada wa dola bilioni moja kwa Afghanistan na kutishia kupunguza zaidi aina zote za ushirikiano na taifa hilo baada ya wanasiasa hasimu nchini humo kushindwa kukubaliana kuunda serikali mpya.

https://p.dw.com/p/3ZxBj
US-Außenminister Pompeo in Afghanistan mit Aschraf Ghani
Picha: picture-alliance/dpa/Afghan Presidential Palace

Uamuzi huo wa Marekani umetangazwa siku ya Jumatatu na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo Mike Pompeo aliyefanya ziara ambayo haikutangazwa mjini Kabul.


Pompeo alifanya ziara hiyo kwa lengo la kukutana na wanasiasa hasimu nchini humo ambao ni rais Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah ambao wote wamejitangaza kuwa marais baada ya uchaguzi uliozozaniwa wa mwaka uliopita.

Wakati wa ziara hiyo Pompeo alitumai ataweza kumaliza mkwamo wa kisasa uliopo lakini hakufanikiwa.


Katika taarifa yenye matamshi makali Pompeo amenyooshea kidole cha lawama wanasiasa hao wawili kwa kushindwa kufanya kazi pamoja hatua inayotishia kuuweka rehani mkataba wa amani utakaowezesha kumaliza mzozo wa muda mrefu nchini humo.


Mkataba wa amani kati ya Marekani na kundi la wanamgambo wa Taliban la nchini Afghanistan umetoa matumaini ya kumaliza ushiriki wa Marekani na majeshi yake nchini Afghanistan tangu ilipojitumbukiza kwenye mzozo huo mwaka 2001.

US-Außenminister Pompeo in Afghanistan mit Abdullah Abdullah
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo akiwa katika mkutano na hasimu wa rais Ghani Abdullah Abdullah, aliejitangaza pia kuwa rais.Picha: picture-alliance/dpa/Sepidar Palace

Marekani yaelza kuvunjwa moyo na Ghani na Abdullah


Kuhusu msaada ambao Marekani imetangaza kuuondoa, Pompeo amekataa kutoa ufafanuzi jinsi utakavyopunguzwa au iwapo Marekani imeweka muda wa mwisho kwa wanasiasa hao kufikia makubalino ya kumaliza mvutano.


Pompeo amesema Marekani imevunjwa moyo na wanasiasa hao wawili aliosema wameutia doa uhusiano kati ya Washignton na Kabul na muungano wa washirika waliojitolea maisha kufanikisha ujenzi wa hatma mpya ya Afghanistan.


Lakini akizungumza na waandishi habari akiwa njiani kurejea Washington, Pompeo amesema ana matumaini kuwa Ghani na Abdullah watashughulikia tofauti walizo nazo na Marekani haitolazimika kuifutia misaada nchi hiyo.


Wakati wa safari yake mwanadiplomasia huyo wa Marekani alisimama pia nchini Qatar alikokutana kwa mazungumzo na afisa mwandamizi wa kundi la Taliban na kurejea matamshi yake kuwa Ghani na Abdullah wanakwenda kinyume na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Taliban.

Bildkombo Abdullah Abdullah und Aschraf Ghani
Abdullah Abdullah na rais Ashraf Ghani wameshindwa kufikia muafaka hatua iliyoipelekea Marekani kuipunguzia msaada Afghnaistan.


Mkataba huo  pamoja na na mambo mengine ulitoa wito wa kuanza mazungumzo ya amani ndani ya Afghanistan mnamo Machi 10 lakini hilo halikufanikiwa.


Hadi sasa Ghani na Abdullah bado hawajaafikiana kuhusu wajumbe watakaoiwakilisha serikali kwenye mazungumzo hayo wala kufikia mwafaka wa kubadilishana wafungwa na kundi la Taliban kama ilivyoelekezwa ndani ya makubaliano na kundi hilo.


Katika hatua nyingine, Pompeo amesema Marekani itaendelea na mipango ya kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Afghnasitan chini ya makubaliano ya mkataba wa amani na Taliban unaotaka nchini hiyo ipunguze idadi ya wanajeshi wake hadi 8,600 kutoka 13,000 waliopo sasa.


Kuhusu mzozo wa kisiasa nchini Afghanistan, bado haijawa wazi namna utatatuliwa.


Licha kuwa tume ya uchaguzi ilimtangaza Ghani kuwa mshindi wak uchaguzi uliopita, hasimu wake Abdullal Abdullah amelalamika juu ya kuwepo mizengwe na makosa mengi wakati wa zoezi la kupiga kura na kutangaza mshindi.

Chanzo: Mashirika