1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yafanya mashambulizi mapya Iraq

10 Agosti 2014

Rais Barack Obama wa Marekani Jumamosi (09.08.2014) amesema mashambulizi ya anga ya Marekanni yameteketeza silaha na zana ambazo waasi wa Dola la Kiislamu wangeliweza kuzitumia kushambulia Arbil.

https://p.dw.com/p/1Crw2
Rais Barack Obama wa Marekani akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya Marekani. (09.08.2014)
Rais Barack Obama wa Marekani akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya Marekani. (09.08.2014)Picha: Getty Images

Amewaambia waandishi wa habari kabla ya kuondoka Washington kuelekea Massachusetts kwa mapumziko ya wiki mbili kwamba "Sifikiri tutalitatuwa tatizo hili katika kipindi cha wiki kadhaa.Suala hili litachukuwa muda kidogo"

Obama amesema Marekani itaendelea kutowa msaada wa kijeshi na ushauri kwa serikali ya Iraq na vikosi vya Wakurdi lakini amesisitiza mara kwa mara umuhimu kwa Iraq kuunda serikali yake yenyewe yenye ushirikishi.

Waziri wa mambo ya nje wa Iraq Hoshyar Zebari ameuambia mkutano wa waandishi wa habari jana usiku kwamba timu ya kijeshi ya Marekani pia hivi sasa iko katika mji mkuu wa Wakurdi wa Arbil kutowa ushirikiano wake wa kiufundi kwa vikosi vya Wakurdi vya "Peshmerga.Amesema mashambulizi hayo yaliokusudia kudhoofisha uwezo wa kile alichosema magaidi hao na kupata ushindi wa kimkakati yamekuwa na ufanisi mkubwa.

Mashambulizi mapya

Hayo ni mashambulizi mapya tokea Rais Barack Obama wa Marekani alipoamuru hapo Alhamisi kufanyika mashambulizi dhidi ya kundi hilo lililojitenga na Al Qaeda ambalo limeyateka maeneo mengi ya Iraq na kutowa vitisho kwa Wakristo na makundi mengine ya kidini.

Ndege ya kivita chapa ya Super Homet.
Ndege ya kivita chapa ya Super Homet.Picha: picture-alliance/dpa

Obama amesema mashambulizi hayo yalioanza Ijumaa yanaweza kuzuwiya kitendo cha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya wachache waliopotezewa makaazi yao wakiwemo maelfu ya Wayazidi waliokwama kwenye mlima wa Sinjar bila ya kuwa na chakula au maji.

Akizungumza katika hotuba yake ya kila wiki kwa njia ya radio Jumamosi Obama amesema kikosi cha anga cha Marekani kitaendelea kulishambulia kundi hilo la wanamgambo linalojiita Dola ya Kiislamu iwapo ikibidi.

Kulinda raia wa Marekani

Amesisitiza haja ya kuwalinda raia wa Marekani wanaofanya kazi nchini Iraq na kusema kwamba Marekani itaendelea kufanya kile inachoweza kuwasaidia maelfu ya jamii ya kidini ya wachache ya Yazidi ambao wamekwama katika Mlima Sinjar bila ya kuwa na chakula au maji baada ya kukimbia mashambulizi ya wanamgambo hao wa itikadi kali wanaoendelea kuteka miji nchini Iraq.

Kikosi cha Wakurdi cha Peshmerga kikiwa katika mstari wa mbele wa mapambano katika jimbo lao la Kurdistan. (08.08.2014)
Kikosi cha Wakurdi cha Peshmerga kikiwa katika mstari wa mbele wa mapambano katika jimbo lao la Kurdistan. (08.08.2014)Picha: Reuters

Amesema maelfu ya wanaume, wanawake na watoto ambao wamekimbilia kwenye mlima huo wiki moja iliopita wanakufa kutokana na njaa na kiu. Ameongeza kusema kwamba pia ameamuru mashambulizi ya anga ya Marekani kuwalenga watu maalum ili kuvisaidia vikosi vya Iraq kuwaokowa watu na familia zao waliozingirwa na waasi.

Hata hivyo akiwa kama Amiri Jeshi Mkuu amesisitiza kwamba hatoamuru vikosi vya Marekani vya ardhini kurudi tena nchini Iraq kupambana na kundi hilo la Dola la Kiislamu na pia ameelezea nia yake ya kutoliachia kufanikisha lengo lao la kuanzisha taifa la Kiislamu katika ardhi ya Iraq na Syria.

Marekani iliongoza uvamizi nchini Iraq hapo mwaka 2003 na kupigana vita vilivyomn'gowa dikteta Saddam Hussein. Hata hivyo Obama aliviondowa vikosi vyote vya Marekani kutoka Iraq hapo mwaka 2011 baada ya umma wa Marekani uliochoshwa na vita kuzidi kuwa na mashaka juu ya harakati za kijeshi za Marekani nchi za nje.

Serikali shirikishi ndio ufumbuzi

Kuendelea kupamba moto kwa machafuko nchini humo kunakuja wakati Iraq ikizidi kuzongwa na mkwamo mkubwa unaotokana na kushindwa kwa makundi ya kisiasa kufikia muafaka juu ya mtu wa kushika wadhifa wa uwaziri mkuu.

Maelfu ya Wayazidi walionasa kwenye milima ya Sinjar. (09.08.214)
Maelfu ya Wayazidi walionasa kwenye milima ya Sinjar. (09.08.214)Picha: picture alliance/AA

Ikulu ya Marekani inasisitiza wakati mashambulizi hayo ya anga yumkini yakaweza kuwadhibiti wanamgambo hao katika kipindi cha muda mfupi, suluhisho pekee la kudumu kwa mzozo wa Iraq ni kwa jamii zilioko nchini humo kupatana na kwa viongozi wa kisiasa kufanya juhudi kubwa zaidi kupunguza tafauti zao.

Wapiganaji wa Dola la Kiislamu wameteka sehemu kubwa ya ardhi ya Iraq katika wiki za hivi karibuni ukiwemo mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Mosul. Wiki iliopita wanamgambo wa kundi hilo walianza kuelekea upande wa kaskazini lilioko jimbo lenye mamlaka ya ndani la Wakurdi ambalo linapakana na Uturuki.

Mwishoni mwa mwezi wa Juni kiongozi wa kundi hilo la Dola la Kiislamu Abu Bakr al- Baghdadi alijitangaza kuwa khalifa na kuundwa kwa dola hiyo itakayoongozwa kwa misingi ya Kiislamu katika maeneo yalioko chini ya udhibiti wa wapiganaji wake wa jihadi nchini Iraq na Syria.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/dpa

Mhariri : Sudi Mnette