1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Wademocrat wapitisha bajeti isiyojumuisha ukuta

Daniel Gakuba
4 Januari 2019

Wabunge wa chama cha Democratic wanaolidhibiti Baraza la Wawakilishi tangu jana, wamepitisha mpango wa kuzifungua shughuli za serikali ya nchi hiyo zilizokwama, bila kujumuisha ujenzi wa ukuta unaotakiwa na Rais Trump.

https://p.dw.com/p/3B1sS
USA Washington - 116 Kongresssitzung: Nancy Pelosi
Picha: Reuters/K. Lamarque

 

Mpango huo wa Wademocrat ulipitishwa kwa kura 239 dhidi ya 192 zilizoupinga, kura hizo kwa sehemu kubwa zikifuata msitari wa vyama. Haukujumuisha dola bilioni 5 zinazotakiwa na Rais Donald Trump kwa ajili ya ujenzi wa ukuta kwenye mpaka kati ya Marekani na Mexico, ambao ni ahadi muhimu ya kampeni yake.

Tayari Warepublican wanaolidhibiti baraza la Seneti wamesema bayana hawataridhia mpango wowote usioheshimu masharti ya Rais Trump, na rais huyo mwenyewe anashikilia msimamo huo huo wa kutousaini mpango wowote wa matumizi ya serikali usiohusisha ujenzi wa ukuta.

Ukuta kati ya ukweli na upotoshaji

Washington Kongress konstituierende Sitzung Pelosi
Nancy Pelosi, Spika mpya wa Baraza la Wawakilishi, MarekaniPicha: Getty Images/W. McNamee

Spika mpya wa Baraza la seneti, Nancy Pelosi, akitoa sababu ya wao kutokubali rai ya Rais Trump ya ujenzi wa ukuta, amesema ukuta kati ya Marekani na Mexico ni kinyume na maadili ya Marekani, na kuongeza kuwa badala ya kusaidia kuimarisha usalama wa taifa lao, ukuta huo unatumiwa na Trump kuwaziba watu macho.

''Ni ukuta kati ya wafuasi wake na ukweli, ambao hataki waujue. Kuhusu sera zake juu ya bima ya afya na mfumo ya mafao ya kijamii, hataki wajue sera yake kuhusu kulinda maji safi na hewa safi katika wizara ya mazingira.'' Amesema Pelosi na kumshutumu Trump ''kutaka watu wapumbazwe na mazungumzo kuhusu ukuta.'' 

Rais Trump alifanya mazungumzo na viongozi wa vyama bungeni katika Ikulu ya White House Juzi Jumatano, ambayo yaliambulia patupu, na amewaalika tena hii leo kwa mazungumzo mengine ya kutafuta muafaka juu ya suala hilo tete la ujenzi wa ukuta mpakani. Maafisa wa Ikulu hiyo wanaamini kwamba mara hii mjadala huo unaweza kupiga hatua, kwa sababu Bi Pelosi tayari amekwishachukua rasmi madaraka ya uspika.

Taifa lililogawanyika

Kama ilivyo miongoni mwa viongozi, maoni miongoni mwa umma wa kimarekani yamegawanyika sana kuhusu ukuta huo wa mpakani. Uchunguzi wa maoni unaonyesha kwamba walio wengi wanaupinga, lakini unaungwa mkono vilivyo na wafuasi sugu wa rais Trump.

Mkwamo huu umeziathiri wizara nane za serikali ya Marekani na wafanyakazi zaidi ya laki nane wa wizara hizo, ambao wamelazimika kubaki nyumbani, au kufanya kazi bila malipo.

Hakuna dalili za ufumbuzi wa mzozo huo, kwa sababu kila upande unang'ang'ania msimamo wake, ukitiwa shime na wafuasi wake kisiasa.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre,ape

Mhariri: Mohammed Khelef