1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Urusi zakubaliana kuhusu Syria

16 Desemba 2015

Marekani na Urusi zimekubaliana kuendeleza juhudi za kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, huku duru mpya ya mazungumzo ya kimataifa ya amani ikitarajiwa kuandaliwa Ijumaa wiki hii mjini New York, Marekani

https://p.dw.com/p/1HO0z
Russland USA John Kerry & Sergej Lawrow in Moskau
Picha: Reuters/M. Zmeyev

Baada ya mkutano wa karibu saa tatu mjini Moscow baina ya Rais wa Urusi Vladmir Putin na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry, pande hizo mbili zilionekana kukarabia kukubaliana na msimamo wa kila mmoja kuhusu Syria, ijapokuwa kuna tofauti ambazo bado zipo kuhusu hatima ya Rais Bashar al-Assad. Lakini viongozi hao wawili walikubaliana kuwa tofauti zao hazistahili kuvuruga mazungumzo ya kisiasa kuhusu mustakabali wa Syria. Huyu hapa waziri Kerry "Wakati hatuonani uso kwa uso katika kila suala kuhusu Syria, leo hakika tumekubaliana, na Rais Putin alikubali, kuwa kimsingi tunaiona Syria katika njia sawa. tunataka matokeo hayo hayo. tunaiona hatari hiyo hiyo. Tunaelewa changamoto zile zile. na sote tunaamini kuwa Syria yenye umoja, isiyogawika kwa ajili ya madhehebu ya kidini inawakilisha mustakabali, na tunakubaliana pia kuwa ni mustakabali usiokuwa na IS".

Mazungumzo hayo kimataifa yanayopangwa Ijumaa wiki hii, jijini New York, yanalenga kutafuta azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha mchakato wa kupatikana mpango wa kusitishwa mapigano na kuanzishwa mazungumzo ya amani baina ya utawala wa Assad na upinzani unaopambana na serikali yake. Marekani inaitegemea Urusi kumshawishi mshirika wake Assad kujiunga kwenye meza ya mazungumzo na waasi wa upinzani.

Saudi-Arabien - Treffen der Syrischen Opposition in Riad
Upinzani wa Syria ulikutana nchini Saudi ArabiaPicha: Getty Images/AFP/F. Nureldine

Lakini suala linalovuruga juhudi hizo ni kitisho kinachosababishwa na kundi la Dola la Kiislamu kueneza harakati zake nje ya mipaka ya Syria.

Jerry anatumai kuwa ikiwa utawala wa Assad na waasi watakubali kusitisha mapigano, basi, Urusi na muungano wa washirika wa nchi za magharibi na Kiarabu unaoongozwa na Marekani wanaweza kuyaelekeza mashambulizi yao kwa wapiganaji hao wa jihadi. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema nchi hizo mbili zimekubaliana kuimarisha juhudi dhidi ya ugaidi. "tumekubaliana kuendelea kufanya kazi, ambayo tayari imepiga hatua kubwa, kazi ya kutayarisha orodha moja ya mashrika ya kigaidi na kuusaidia Umoja wa Mataifa katika kuunda ujumbe wa upinzani unaoyashirikisha makundi yote ambao utakuwa tayari kufanya mazungumzo muhimu na ujumbe wa serikali ya Syria, ndani ya misingi iliyokubaliwa na wanachama wa kikundi cha kimataifa kinachoiunga mkono Syria".

Mazungumzo hayo yalikuwa mashakani baada ya Urusi kukasirishwa na mazungumzo ambayo hayakutarajiwa yaliyoandaliwa Saudi Arabia wiki iliyopita, ikisema kuwa makundi kadhaa ya “kigaidi” yalishiriki. Katika mkutano uliofanyika Riyadh, waasi walisisitiza kuwa Assad na washirika wake waondoke madarakani, “katika mwanzo wa kipindi cha mpito” kilichotangazwa mjini Vienna mwezi uliopita na mataifa yenye nguvu duniani.

Maafisa wa Marekani wanasisitiza kuwa Urusi imejitolea katika mpango wa mpito wa kisiasa ili kumaliza vita na kuonya kuwa ikiwa haitamleta Assad kwenye meza ya mazungumzo, majeshi ya Urusi yatadhoofishwa katika mapigano hayo. Urusi imepeleka majeshi ya angani na majini nchini Syria kuunga mkono utawala wa Assad, wakati Marekani na washirika wake wakizilipua ngome za IS nchini Syria na Iraq.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Iddi Ssessanga