1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani njia panda katika vita dhidi ya IS

29 Julai 2015

Marekani inajikuta katika njia panda kufuatia mvutano unaoendelea kati ya Uturuki na Wakurdi katika vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS. Pande zote mbili ni washirika muhimu wa Marekani Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/1G6pr
Türkei Luftangriffe auf Kurden in Syrien
Mashambulizi ya angani ya Uturuki dhidi ya PKK nchini SyriaPicha: Reuters/M. Sezer

Licha ya pande zote mbili kuwa washirika muhimu wa Marekani katika kuyafikia malengo yake Mashariki ya Kati, sasa zinapingana vikali huku kila upande ukiulaumu mwingine. Uturuki imefanya mashambulizi ya mabomu dhidi ya ngome za Wakurdi nchini Iraq ambayo yumkini yakavuruga vita vya Marekani dhidi ya Dola la Kiislamu.

Kwa mujibu wa serikali ya Uturuki hakuna tofauti kati ya kundi la Dola la Kiislamu IS na kundi la wanamgambo wa Kikurdi la PKK. Makundi yote mawili ni ya kigaidi. "Kundi lolote linalosababisha kitisho kwa mipaka ya Jamhuri ya Uturuki, hatua zitachukuliwa bila kusitasita," amesema waziri mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, baada ya Uturuki kuanzisha operesheni dhidi ya makundi hayo. "Hakuna anayetakiwa kuwa na shaka."

Lakini kundi la PKK limedhihirisha kuwa adui hatari kwa kundi la Dola la Kiislamu kwa mujibu wa Michael Gunter, ambaye ameandika vitabu kadhaa juu ya Wakurdi. Kundi la PKK limefaulu sana katika kulikabili kundi la Dola la Kiislamu kiasi kwamba kumetolewa miito nchini Marekani kuliondoa kutoka orodha ya makundi ya kigaidi ya wizara ya nje ya nchi hiyo.

"Marekani inapaswa ifanye hivyo," amesema Gunter, profesa katika chuo kikuu cha Teknolojia cha Tennessee, wakati alipozungumza na DW. "Marekani imekuwa ikilisaidia kundi la PKK kwa kukidhamini chama cha Demokrasia cha Wakurdi, PYD, nchini Syria, ambacho kina mafungamano na kundi la PKK."

Kurden drängen IS im Sinjar-Gebirge zurück 20.12.2014
PKK walikuwa na jukumu muhimu kuwaokoa WayazidiPicha: Reuters/Massoud Mohammed

Kundi la PKK pamoja na Marekani zimejikuta upande mmoja sio tu nchini Syria pekee. Wakati wanamgambo wa Dola la Kiislamu walipowazingira maelfu ya Wayazidi katika milima ya Sinjar kaskazini mwa Iraq mwaka uliopita, rais wa Marekani Barack Obama aliwaambia Wamarekani kwamba utawala wake ulikuwa na jukumu la kuwaokoa watu hao wa kundi dogo la kidini kutokana na mauaji ya kiholela waliokuwa wakiteswa.

Matokeo yake Marekani ikaanza kampeni ya mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya Dola la Kiislamu, lakini sio Marekani iliyowaokoa Wayazidi wa Sinjar. Ni wapiganaji wa PKK waliosaidia kuwaondoa kutoka milima hiyo na kuwasindikiza katika maeneo salama.

Mashambulizi dhidi ya IS ni njama

Sasa Uturuki kwa uwazi imejiingiza katika vita vya Iraq na Syria ambavyo vinazidi kuwa vigumu kila uchao. Wiki iliyopita mshambuliaji wa kujitoa muhanga wa Dola la Kiislamu aliwaua wanaharakati 32 katika mji wa kaskazini wa Suruc, karibu na mpaka na Syria. Kwa kulipiza kisasi, waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu alianzisha mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya Dola la Kiislamu kwa mara ya kwanza na imeiruhusu Marekani kutumia kambi yake jeshi ya Incirlik.

Shambulizi hili ni njama tu, hamaanishi," amesema Gunter na kuongeza kuwa Uturuki kimsingi inalitumia kundi la Dola la Kiislamu kama silaha dhidi ya Wakurdi wa Syria. "Imeorodheshwa vizuri sana kwa miaka miwili iliyopita kwamba Uturuki imewaruhusu wapiganaji wa Jihad wanaoliunga mkono kundi la Dola la Kiislamu kutoka maeneo yote ya ulimwengu kusafiri kupitia Uturuki kwenda Syria na kujiunga na kundi hilo," akaongeza kusema Gunter.

Kampfjet Türkei
Uturuki imezilenga ngome za IS na PKKPicha: picture-alliance/AA

Serikali ya Uturuki wakati huo huo imeanzisha mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya ngome za PKK kaskazini mwa Iraq. Inaripotiwa wanamgambo wa kundi hilo walikuwa wamewaua maafisa wawili wa polisi nchini Uturuki, wakiulaumu utawala wa mjini Ankara kwa kuufumbia macho uhalifu unaofanywa na Dola la Kiislamu dhidi ya Wakurdi.

Marekani imeyaunga mkono mashambulizi ya Uturuki dhidi ya PKK. Katika mkutano na waandishi wa habari msemaji wa wizara ya mambo ya nje John Kirby aliliita kundi hilo kuwa la kigaidi na kusema Uturuki ina haki ya kujilinda. Gunter amesema, "Ni ujinga kwamba Marekani haiwezi kuliona hili. Uturuki inawaua Wakurdi wanaopigana na Dola la Kiislamu, kundi ambalo linatakiwa kuwa adui wa Marekani.

Mwandishi:Josephat Charo/dw.com/english

Mhariri:Iddi Sessanga