1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi kusitisha mapigano Syria

23 Februari 2016

Marekani na Urusi zimetangaza makubaliano ya kihistoria ya kusitisha mapigano Syria kuanzia Jumamosi ijayo. Makubaliano hayo yamekosolewa na waasi wa Syria kwa kutoyajumulisha makundi yote yanayohusika na mzozo huo.

https://p.dw.com/p/1I0Bx
Syrien Bombenanschlag in Homs
Wasyria wakiwa wamekusanyika eneo lililoshambuliwa kwa mabomu mawili kitongoji cha Al-Zahraa mjini HomsPicha: Stringer/AFP/Getty Images

Katika taarifa ya pamoja jana (22.02.2016) Marekani na Urusi zilisema makubaliano ya kusitisha mapigano yataanza Ijumaa saa sita usiku saa za Damascus, na hivyo kusitisha mapigano makali yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 260,000 na nusu ya wakazi wa Syria wakiyahama makazi yao.

Rais wa Marekani Barack Obama na rais wa Urusi Vladimir Putin waliyajadili makubaliano hayo kwa njia simu. Yatayajumuisha makundi yanayohusika katika mzozo wa Syria mbali na kundi la Dola la Kiislamu na Al Nusra Front na pande zote zinazotaka kushiriki sharti zifanye hivyo kabla Ijumaa saa sita mchana.

Rais Putin aliyaeleza makubaliano hayo kuwa ni hatua halisi kuelekea kusitisha umwagaji damu na inaweza kuwa mfano wa kuigwa dhidi ya ugaidi. "Upinzani utaacha kupigana na jamhuri ya Syria na makundi unayoyafadhili. Kwa makundi kama Dola la Kiislamu, Al Nusra Front, na mengine ya kigaidi yanayotambuliwa hivyo na Umoja wa Mataifa, hayahusiki kabisa na makubaliano haya. Mashambulizi dhidi yao yataendelea."

Russland Wladimir Putin
Rais wa Urusi, Vladimir PutinPicha: Reuters/S. Ilnitsky

Rais Putin aidha alisema Urusi itaendelea kushirikiana na serikali halali ya Syria mjini Damascus kuhakikisha inayaheshimu makubaliano hayo na wanatarajia kwamba Marekani itafanya hivyo hivyo na washirika wake na makundi inayoyaunga mkono.

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry alisema iwapo makubaliano hayo yatatekelezwa, machafuko yatapungua na kutanua usafirishaji wa mahitaji ya kibinaadamu katika maeneo yanayozingirwa na kuunga mkono kipindi cha mpito kuelekea kuundwa serikali itakayoyashughulikia masilahi ya watu wa Syria.

Maoni mbalimbali yajitokeza

Kundi kuu la upinzani la Syria lilisema linayaunga mkono makubaliano hayo kwa masharti kwamba miji isizingirwe, wafungwa waachiwe huru, mashambulizi ya mabomu dhidi ya raia yakome na misaada ya kibinaadamu iruhusiwe.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mzozo wa Syria Staffan de Mistura aliyapongeza makubaliano ya usitishwaji mapigano akisema ataanzisha kikosi maalumu kusaidia kuyasimamia yatakapoanza kutekelezwa. "Hatua nyingine inayofuata ni kuhakikisha kati ya sasa na wakati usitishwaji mapigano utakapoanza rasmi, washikadau wote waliohusika katika mzozo huu, wanashirikishwa na wanajitolea kwa dhati kuuheshimu."

De Mistura alidokeza kutafanyika mkutano mjini Geneva hivi karibuni mapigano yatakapositishwa kwa lengo la kuendeleza mchakato wa kutafuta suluhisho la mzozo wa Syria.

Syrien Staffan de Mistura UNO-Gesandter für Syrien
Staffan de MisturaPicha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alisema makubaliano hayo ni ishara ya matumaini na amezitaka pande zote husika ziyaheshimu.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel Moshe Yaalon alisema ana shaka kama makubaliano ya kusitisha mapigano yatafaulu bila kulijumuisha kundi la Dola la Kiislamu na Al Nusra Front.

Kwa upande waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Philip Hammond alisema yatafaulu tu kama kutakuwa na mabadiliko makubwa ya tabia kwa upande wa utawala wa Syria na Urusi, inayotakiwa ikomeshe mashambulizi dhidi ya raia na makundi ya upinzani yenye msimamo wa wastani.

Tangazo la kusitisha mapigano Syria lilitolewa siku moja baada ya kundi la Dola la Kiislamu kudai kuhusika na mashambulizi mawili ya mabomu katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali yaliyowaua watu zaidi ya 134 karibu na eneo takatifu kusini mwa Damascus na wengine wapatao 64 mjini Homs.

Muda mfupi baada ya tangazo hilo rais wa Syria Bashar al Assad alitangaza uchaguzi wa bunge utafanyika Aprili 13 mwaka huu.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/rtre/dpae

Mhariri:Daniel Gakuba