Marekani na Uingereza zashinikiza vikwazo dhidi ya Sudan Kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani na Uingereza zashinikiza vikwazo dhidi ya Sudan Kusini

Marekani na Uingereza zimeanza mazungumzo katika vikao vya Umoja wa Mataifa kushinikiza vikwazo dhidi ya serikali ya Sudan Kusini kwa kushindwa kusaini mkataba wa amani unaonuiwa kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Susan Rice

Susan Rice, Mshauri wa masuala ya usalama wa kitaifa, Marekani

Marekani na Uingereza zimeanza mazungumzo katika vikao vya Umoja wa Mataifa kushinikiza vikwazo dhidi ya serikali ya Sudan Kusini kwa kushindwa kusaini mkataba wa amani unaonuiwa kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili sasa.

Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar alisaini makubaliano hayo ya Jumatatu mjini Addis Ababa Ethiopia, lakini rais Salva Kiir akasema anahitaji muda kuyapitia.

Mshauri wa masuala ya usalama wa kitaifa wa Marekani, Susan Rice, ameishutumu serikali ya Salva Kiir kwa uongozi ulioshindwa, na kusema imepuuza fursa nyingine muhimu ya kuumaliza mzozo ambao umewaua maelfu ya watu na kuitumbukiza nchi hiyo changa duniani katika machafuko ya umwagaji damu.

"Lazima hatua zichukuliwe dhidi ya wale wanaoendelea kuzikwamisha juhudi za amani," akasema Rice huku akilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liiwekee vikwazo serikali ya Sudan Kusini iwapo haitasaini makubaliano hayo katika siku 15 zijazo.

Katika hotuba yake mbele ya baraza la usalama hapo jana naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa David Pressman aliileza hatua ya rais Kiir kushindwa kusaini mkataba wa amani kuwa ya kughadhabisha.

Südsudan Präsident Salva Kiir

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir akiwa Addis Ababa (17.08.2015)

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema katika taarifa kwamba kiongozi huyo ana matumaini makubwa rais Kiir atasaini makubaliano ya Addis Ababa kabla kipindi cha siku 15 kumalizika na ametoa mwito mapigano yanayoendelea Sudan Kusini yakome ana amani idumishwe.

Akizungumza jana katika mkutano wa baraza la usalama kudumisha amani na usalama wa kimatiafa, Ban Ki Moon alisema, "Umoja wa Mataifa unashirikiana na mashirika ya kikanda kugawana majuku katika kulinda amani na usalama. Tunatakiwa tufanye kila liwezekanalo kuwasaidia kutatua matatizo ya kikanda na kuzishirikisha nchi husika katika kutafuta suluhisho."

Hatua za kuchukuliwa zajadaliwa

Wakati wa ziara yake ya hivi karibuni Afrika Mashariki rais wa Marekani Barack Obama aliziunga mkono juhudi za amani Sudan Kusini, taifa ambalo Marekani ilichangia katika mchakato wa kuundwa kwake, lakini ambalo wakosoaji wanasema sasa limetelekezwa.

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York mataifa yanatafakari juu ya hatua ya kuchukua dhidi ya Sudan Kusini. Naibu balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Peter Wilson, ameliambia baraza la usalama la umoja huo "Ikiwa serikali ya Sudan Kusini haitotia saini mkataba huu uliosimamiwa na jumuiya ya IGAD, basi lazima tuwe na msimamo wa pamoja juu ya hatua tunazotaka kuchukua. Hatuwezi kukaa kitako huku viongozi wakiendelea kupigana na mateso yanayowakabili watu wao yakiendelea kuongezeka."

Duru kadhaa za mazungumzo zimefeli kuyamaliza mapigano ambayo yamewaua watu zaidi ya 10,000 na kuwalazimisha wengine zaidi ya milioni mbili kuyakimbia makazi yao, huku pande zote mbili katika mzozo huo zikiendelea kupigana licha ya kusainiwa mikataba kadhaa ya kusitisha mapigano.

Mwandishi:Josephat Charo/reuters/afp/ap

Mhariri:Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com