Marekani kuweka wanajeshi zaidi Ulaya Mashariki | NRS-Import | DW | 31.03.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Marekani kuweka wanajeshi zaidi Ulaya Mashariki

Marekani itajiimarisha kijeshi katika nchi za Ulaya ya mashariki kwa kuongeza idadi ya wanajeshi wake, ili kukabili inachoita uvamizi wa Urusi. Marekani imesema itaongeza brigedi moja , yaani askari zaidi ya 4000

Kamanda wa majeshi ya Marekani barani Ulaya Jenerali Philip Breedlove

Kamanda wa majeshi ya Marekani barani Ulaya Jenerali Philip Breedlove

Kamanda wa majeshi ya Marekani barani Ulaya Jenerali Philip Breedlove amesema kuongeza wanajeshi katika nchi za Ulaya Mashariki kunathibitisha msimamo thabiti wa Marekani wa kuwapa uhakika washirika wake wa kijeshi katika mfungamano wa NATO.

Sera ya kuendelea kuvibadilisha vikosi itakayoanza mapema mwaka ujao itaongeza uwepo wa majeshi ya Marekani barani Ulaya hadi brigedi tatu zenye uwezo kamili wa kupambana. Jenerali Breedlove ameeleza kuwa washirika wa NATO wataweza kuona uwepo zaidi wa brigedi za kisasa katika nchi zao.

Ulaya Mashariki yaunga mkono

Viongozi wa nchi za Ulaya Mashariki wameunga mkono uamuzi huo wa Marekani. Waziri wa ulinzi wa Latvia Raiomonds Bergmanis amesema uamuzi wa Marekani kuongeza majeshi katika nchi za Ulaya Mashariki unathibitisha ahadi aliyoitoa Rais Barack Obama katika hotuba yake ya Tallinn, mji mkuu wa Estonia mnamo mwaka wa 2014. Obama alisema wakati huo kuwa ni muhimu kuilinda miji ya Ulaya Mshariki kama ilivyo muhimu kuilinda miji ya Berlin, London na Paris.

Waziri wa ulinzi wa Poland Antoni Macierewicz pia ameuinga mkono hatua ya Marekani. Amesema kuimarisha uwepo na uwezo wa majeshi ya Marekani barani Ulaya ni hatua muhimu. Ameeleza kuwa juhudi zote za serikali zilizolenga shabaha ya kuhakikisha uwepo wa majeshi ya NATO na ya Marekani katika Ulaya Mshariki zimezaa matunda.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter

Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter

Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter mwezi uliopita alizindua bajeti ya wizara yake kwa ajili ya mwaka ujao yenye nyongeza ya kiasi cha Dola Bilioni 3.4 yaani mara nne ya bajeti ya mwaka uliopita. Bajeti hiyo itagharimia kinachoitwa mpango wa kuwapa tena uhakika washirika wa NATO wa barani Ulaya.

Lengo ni kuizuia Urusi kuendelea kupora ardhi za nchi nyingine baada ya kuliteka jimbo la Ukraine la Krimea mnamo mwaka wa 2014 na kuliingiza katika himaya yake. Waziri wa ulinzi wa Marakeni Ashton Carter amesema nchi yake imeeleza wazi kwamba itayalinda maslahi yake, washirika wake na misingi ya mfumo wa dunia.

Baadhi ya wanachama wana mashaka

Hata hivyo baadhi ya wanachama wa NATO wa barani Ulaya, kama Ujerumani wana mashaka juu ya kuwekwa kwa idadi kubwa ya askari barani Ulaya katika mpangilio wa kudumu. Ujerumani imesema hatua hiyo inaweza kukiuka makubaliano ya mwaka wa 1997 yaliyofikiwa baina ya NATO na Urusi.Lakini hatua inayochukuliwa na Marekani sasa inaepuka mkataba huo kwa sababu majeshi hayo hayatawekwa daima katika Ulaya Mashariki. Vikosi hivyo vitakuwa vinahamishwa. Kwa sasa Marekani inao wanajeshi 62,000 barani Ulaya.

Urusi imeonya dhidi ya kuwekwa kwa idadi kubwa ya askari wa NATO karibu na mipaka yake.

Mwandishi:Mtullya abdu./afpe/ZA

Mhariri:

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com