Marekani kusambaza vituo vya kijeshi Afrika. | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Marekani kusambaza vituo vya kijeshi Afrika.

Marekani inapanga kusambaza vituo vipya vya kijeshi kwa Afrika katika nchi kadhaa badala ya kuwa na kituo kimoja tu cha makao makuu yake ya kijeshi barani humo.

Rais George W. Bush wa Marekani akiwa katika Wizara ya Ulinzi ya Marekani mjini Washington.

Rais George W. Bush wa Marekani akiwa katika Wizara ya Ulinzi ya Marekani mjini Washington.

Uamuzi huo wa serikali ya Marekani unaonyesha kuongezeka kwa utashi wa mkakati wa Marekani barani Afrika.

Ryan Henry Naibu Mkuu Msaidizi waziri wa ulinzi kwa masual ya sera amewaambia waandishi wa habari wakati akiwa ziarani nchini Algeria kwamba makao hayo ya kijeshi hayatosanifiwa kwa ajili ya kupigana vita bali yatalenga zaidi katika kuvipatia mafunzo vikosi vya usalama vya Afrika.

Amesema wafanyakazi hawatawekwa katika kituo kimoja kikubwa cha makao makuu bali badala yake vituo vitasambazwa katika nchi tafauti barani kote Afrika na vitaratibiwa kwa pamoja.

Henry akiutarifu ubalozi wa Marekani nchini Algeria amesema wako katika hatua za mwisho za uchunguzi yakinifu juu ya kuvitawanya vituo hivyo na kama iwapo hilo litawezekana kabisa hivyo ndivyo wangelipenda kusonga mbele.

Rais George W. Bush wa Marekani ametangaza hapo mwezi wa Februari kwamba alikuwa ametowa idhini ya kuundwa kwa makao mapya ya kijeshi barani Afrika yatakayojulikana kwa jina la Africom ambayo awali yatakuwepo mjini Suttgart Ujerumani lakini baadae yatahamishiwa barani Afrika.

Wachambuzi wa mambo wamesema kwamba mpango huo unaweza kuchukuwa miaka mingi kukamilika kwa sababu mataifa yanayotarajiwa kuwa wenyeji wa vituo hivyo vya kijeshi yumkini yakawa na wasi wasi juu ya kunyanyapaliwa kutokana na kushirikiana na taifa hilo lenye nguvu kubwa kabisa duniani.

Wamesema wakati kunaweza kuwepo kwa hadhi fulani na faida za kiuchumi kwa kuwa mwenyeji wa makao hayo ya kijeshi kituo chochote kile cha kijeshi kitakachoanzishwa na Marekani kinaweza kuwa shabaha ya kushambuliwa na magaidi au serikali wenyeji yenyewe kuvuta nadhari ya kisiasa isiohitajika.

Afisa wa serikali ya Marekani ambaye haruhisiwi kuzungumzia rasmi suala hilo amesema mpango huo wa kuvitawanya vituo vya kijeshi umebuniwa kutokana na ushauri wa mataifa ya Afrika kwamba kuyaweka makao hayo ya kijeshi katika nchi moja huenda kukachochea wivu miongoni mwa mataifa ya Afrika.

Serikali ya Marekani ina wasi wasi kwamba mataifa ya Afrika yenye serikali dhaifu yanatowa nafasi ya kujihifadhi kwa wanamgambo wa Kiislam.

Hivi sasa kambi pekee ya muda mrefu kwa ajili ya wanajeshi wa Marekani barani Afrika ni Kambi la Lemonier ilioko katika nchi ya Afrika Mashariki ya Djibouti.Jeshi la Marekani limegawa baadhi ya shughuli zake duniani kwa makao ya kijeshi ya kanda kama vile Makao ya Central Command yanayoshughulikia Mashariki ya Kati na Pembe ya Afrika.

Kwa mujibu wa mpango mpya kila nchi barani Afrika itakuwa chini ya Makao ya Kijeshi ya Afrika isipokuwa Misri tu ambayo itaendelea kuwa chini ya makao ya Central Command.

Makao hayo mapya kwa Afrika yanatazamiwa kuanza kufanya kazi hapo mwezi wa Septemba mwaka 2008.

Msaidizi huyo waziri wa ulinzi Henry akiwa mwanzoni mwa ziara yake barani Afrika ambayo itamfikisha Morocco,Libya, Misri Djibouti na Ethiopia ambako ndiko yaliko makao makuu ya Umoja wa Afrika amesisitiza kwamba vituo hivyo vya kijeshi haitomaanisha kutumwa kwa wanajeshi zaidi wa ulinzi wa Marekani barani Afrika.

Amesema Marekani inataka nchi za Kiafrika zitimize dhima katika vituo hivyo vya kijeshi ambayo inawafariji.

Algeria mshirika wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi lakini mkosoaji mkubwa wa sera zake za kigeni imedokeza kwamba haitoshiriki kabisa katika kuwa mwenyeji wa vituo hivyo vya kijeshi vya Marekani barani Afrika.

 • Tarehe 11.06.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHCv
 • Tarehe 11.06.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHCv

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com