1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kupunguza kwa nusu kiwango cha gesi chafu

22 Aprili 2021

Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi kupunguza hadi nusu, kiwango cha gesi chafu kinachozalishwa na nchi yake ifikiapo mwaka 2030. Biden ametoa tamko hili alipokuwa anaufungua mkutano wa kilele wa mazingira duniani.

https://p.dw.com/p/3sR6s
Klimakonferenz | Joe Biden
Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Biden amezishinikiza nchi zingine zinazosababisha kutolewa gesi hizo chafu kwa kiwango cha juu, kupunguza ili kwenda sambamba na makubaliano ya kimataifa.

Marekani ni mharibifu mkubwa kabisa wa mazingira kuliko nchi nyengine yoyote duniani lakini lengo hilo lililotolewa na Biden la kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa nusu kiwango kinachotolewa na Marekani kwa sasa, ni jambo ambalo huenda likachochea serikali za nchi zingine kufuata hatua za kupunguza gesi hiyo.

Sifa ya Marekani ilififia wakati wa utawala wa Donald Trump

Kama sehemu ya amri yake ya utendaji aliyoitia saini katika siku zake za kwanza afisini, Biden alitangaza mpango mpya wa mazingira, wa jinsi Marekani itakavyoshirikiana na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani IMF kuzisaidia nchi maskini kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa ajili ya kuyalinda mazingira.

Klimakonferenz | Kanzlerin Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Kay Nietfeld/dpa/Getty Images

Sifa ya Marekani ilififia wakati wa mtangulizi wa Biden, Donald Trump amaye aliiondoa Marekani kutoka kwenye makubaliano ya kimataifa ya Paris ya mwaka 2015, na pia sheria za kulinda mazingira huku akiunga mkono matumizi ya makaa ya mawe, mafuta na gesi.

"Marekani haitosubiri, tumeamua kuchukua hatua kuanzia kwenye serikali kuu, katika miji na majimbo kote nchini. Hatua zitachukuliwa kwenye biashara ndogo ndogo, na kwenye biashara kubwa, pia kwenye mashirika yote na hata wafanyakazi wa Marekani katika nyanja zote," alisema Biden.

Nchi 40 zinazihudhuria zianchangia asilimia 80 ya gesi chafu duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ni miongoni mwa wanaohudhuria mkutano huo na ametoa wito kwa nchi tajiri duniani kutimiza ahadi zao za kufadhili masuala ya mazingira walizotoa katika mkutano wa G7 wa  mwezi Juni mwaka jana.

Mlima Kenya hatarini

Viongozi 40 wanaokutana leo na kesho kwa mkutano huo wa kilele unaoongozwa na Biden, kwa jumla nchi zao zinachangia asilimia 80 ya gesi chafu duniani. Gesi hizo zinaongeza joto ulimwenguni na kusababisha majanga ya ukame, vimbunga na mafuriko miongoni mwa mambo mengine.

Nchi zinazotoa kiwango kidogo cha gesi chafu pia zinahudhuria mkutano huo wa kilele mionmgoni mwa nchi hiyo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamaica na Bangladesh.