1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuongeza ushuru wa bidhaa za China

Lilian Mtono
15 Juni 2018

Marekani inakaribia kukamilisha orodha ya pili ya ushuru unaotarajiwa kufikia dola bilioni 100 kwa bidhaa za China wakati rais Donald Trump akijiandaa kuanza kutekeleza awamu ya mwanzo ya utozaji ushuru.  

https://p.dw.com/p/2zcEK
Donald Trump Pressekonferenz Singapur
Picha: Reuters/J. Ernst

Marekani inakaribia kukamilisha orodha ya pili ya ushuru unaotarajiwa kufikia dola bilioni 100 kwa bidhaa za China, katika wakati ambapo rais Donald Trump akijiandaa kuanza kutekeleza awamu ya mwanzo ya utozaji ushuru ambayo huenda ikasababisha hasira kutoka China.  

China  imeahidi kulipiza kisasi iwapo Marekani itaamua kuziwekea ushuru bidhaa zake. 

Marekani imeandaa orodha ya pili ya bidhaa, wakati ambapo ikiajiandaa kutangaza orodha hiyo hii leo itakayolenga takriban bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 50. Kulingana na maafisa wa serikali, hii ni sehemu ya maamuzi ya Trump ya kuendeleza hatua zake za kuanzisha ushuru wa bidhaa mbalimbali.

Orodha hiyo ya pili itapitia kwenye mchakato wa kawaida utakaohusisha maoni ya umma na kujadiliwa, kama ilivyokuwa kwa orodha ya bidhaa za dola bilioni 50 kwa hivyo huenda ikachukua siku 60 ama zaidi kunaza kutekelezwa. Hayo ni kwa mujibu wa vyanzo vyenye ufahamu kuhusu namna utawala wa rais Trump unavyochukulia masuala yahusuyo ushuru husiana na suala ya ushuru, vilipozungumza na Reuters.

Orodha hiyo inatarajiwa kupunguza athari kwa watumiaji wa bidhaa wa Marekani na wafanyabiashara kwa kuchagua bidhaa ambako kuna mazingira mbadala kutoka mataifa mengine.

China - Außenminister Geng Shuang
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Geng Shuang, amesema China itajibu haraka hatua hizo za Marekani.Picha: picture-alliance/Kyodo

Uchambuzi wa Reuters kuhusu takwimu za ofisi ya Marekani inayohusika na bidhaa zinazoingizwa nchini humo mnamo mwezi Aprili ulionyesha kulikuwa na takriban watumiaji 7,600 na bidhaa za viwanda ambazo zinaweza kuwekewa ushuru kwa thamani ya pamoja ya dola bilioni 101, ambapo China inachangia asilimia 40 ama chini ya kiwango cha bidhaa zinazoingizwa kutoka Marekani kwenda China. 

Hatua hii inatishia kuanzisha upya vita vya kibiashara kati ya Marekani na China.

China kwa upande wake hii leo imeapa kulipiza kisasi mara moja, iwapo Marekani itaendelea azma yake hiyo, ikiwa ni masaa kadhaa baada ya rais Trump kutarajiwa kutangaza mapitio ya ushuru kwenye orodha ya bidhaa za China zenye thamani ya dola bilioni 50.

Marekani na China zilionekana kuelekea kwa kasi kwenye vita vya kibiashara baada ya kusindwa kwa raundi kadhaa za mazungumzo, yaliyolenga kusuluhisha madai ya Marekani dhidi ya sera ya viwanda ya China, upatikanaji wa masoko na pengo la dola bilioni 375 la kibiashara.  

Trump alitarajiwa kuzungumzia hatua hiyo baadae hii leo ya kupitiwa upya kwa orodha ya bidhaa 800, idadi ambayo imeshuka kutoka bidhaa 1,300, hii ikiwa ni kulingana na chanzo kutoka ndani ya serikali ya Trump, mwenye ufahamu kuhusu orodha hiyo. 

Hata hivyo bado haijawa wazi kuhusu wakati ambapo Trump ataanzisha ushuru huo, iwapo ataamua kufanya hivyo. Baadhi ya wadau wa viwanda wameiambia Reuters kwamba wanatarajia hatua hiyo kuanza kuchukuliwa hii leo, kwa kutangazwa rasmi na serikali ama huenda ikasubirishwa hadi wiki ijayo.

China ilichapisha orodha yake binafsi iliyotishia kuziwekea ushuru bidhaa za Marekani zenye thamani ya dola bilioni 50, ambazo ni pamoja na bidhaa za soya, vifaa vya ndege na magari, na ilisema huenda ikalipiza kisasi iwapo Marekani itaendeleza hatua zake.

Trump liahidi kutekeleza mahusiano ya kibiashara aliyoyaita ya haki na China, wakati upungufu wa bidhaa kwenye biashara kati ya mataifa hayo ukiwa umefikia dola bilioni 375 mwaka jana.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman