1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kufungua upya kesi za udhalilishaji wa wafungwa?

24 Agosti 2009

Wizara ya Sheria ya Marekani imependekeza kusikiliza upya baadhi ya kesi zinazohusika na udhalilishaji wa wafungwa na hivyo, wafanyakazi wa CIA na wakandarasi huenda wakashtakiwa kuhusika na vitendo hivyo.

https://p.dw.com/p/JHW1
Attorney General-designate Eric Holder speaks duringa news conference with President-elect Barack Obama, not pictured, in Chicago, Monday, Dec. 1, 2008. (AP Photo/Charles Dharapak)
Mwanasheria Mkuu wa Marekani,Eric Holder.Picha: AP

Kwa mujibu wa Gazeti la New York Times idara ya maadili katika Wizara ya Sheria hivi karibuni ilitoa pendekezo hilo kwa Mwanasheria Mkuu Eric Holder kuzisikiliza upya baadhi ya kesi zinazohusika na udhalilishaji wa wafungwa. Na hii leo ndio Wizara ya Sheria inatoa ripoti inayohusika na habari mpya zilizokusanywa na inspekta mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani-CIA katika mwaka 2004 na hazijawahi kuchapishwa. Ripoti hiyo inatishia kugubika siasa za serikali ya Washington hivi sasa Rais Barack Obama akigombea kuleta mageuzi katika huduma za afya na sera za ulinzi wa mazingira. Obama amesema yeye anajaribu kutazama yale yanayokuja badala ya kutumia wakati mwingi kuchunguza yale yaliyopita.

Gazeti la New York Times likimnukulu mtu aliearfiwa rasmi kuhusu ripoti hiyo bila ya kumtaja kwa jina, limesema CIA ilipopewa ripoti ya uchunguzi uliofanywa na inspekta wake mkuu, iliamua kuwa hakuna hata kesi moja iliyostahili kufunguliwa mashtaka. Lakini mapema mwaka huu Holder aliposhika wadhifa wa Mwanasheria Mkuu chini ya serikali mpya ya Rais Obama na alipoona kuwa tuhuma hizo zimehusika pia na vifo vya watu waliokuwepo kizuizini pamoja na kesi zingine za mateso ya kimwili na kiakili, yeye akaamua kuchukua hatua.Ni dhahiri kuwa kufuatia ripoti ya leo hii na kushauriwa kuwa baadhi ya kesi hizo zifunguliwe upya,hatua thabiti zitachukuliwa na hivyo kuzusha matatizo mapya kwa shirika la ujasusi CIA.

Mapendekezo ya kusikiliza upya kesi hizo hasa yanahusika na tuhuma za udhalilishaji wa wafungwa nchini Iraq na Afghanistan. Ripoti za awali za vyombo vya habari kwa mfano, zinasema kuwa maafisa wa CIA walijaribu kupata habari kwa kutumia bunduki na kekee ya umeme kumtisha kamanda wa al-Qaeda Abd al-Rahim al-Nashiri aliekamatwa Novemba mwaka 2002 na kuzuiliwa miaka minne katika jela moja ya siri ya CIA. Hatimae yeye alikuwa miongoni mwa viongozi watatu wa al-Qaeda walioteswa kwa kumuagiwa maji methali ya kuzamishwa. Ikiwa itaamuliwa kuzisikiliza upya kesi hizo, basi hiyo itakuwa kinyume na vile ilivyoamuliwa na serikali ya rais wa zamani George W.Bush kuzifunga kesi hizo.

Mwandishi: P.Martin /RTR/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman