Marekani kuendelea kuishinikiza Taliban | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani kuendelea kuishinikiza Taliban

Marekani imesema itaendelea kulishinikiza kundi la Taliban kutekeleza ahadi ilizotoa katika mazungumzo ya amani na kwa sasa haitapunguza msaada wa kijeshi kwa wanajeshi wa Afghanistan.

Hayo yamebainishwa siku ya Jumapili na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo na kuongeza kuwa iwapo Taliban haitozingatia ahadi ilizotoa kwa Marekani kwa miezi kadhaa, Rais Donald Trump ataongeza shinikizo na hatopunguza msaada katika vikosi vya usalama vya Afghanistan.

Pompeo ameitoa kauli hiyo katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Marekani, CNN baada ya Rais Trump kusitisha mazungumzo ya amani na Taliban yaliyokuwa yafanyike katika eneo lake la mapumziko la Camp David. Amesema Marekani haitositisha msaada wa kijeshi kwa Afghanistan hadi kundi la Taliban litakapochukua hatua madhubuti na kuonesha kwamba wako makini kuhusu amani.

''Ni juu ya Taliban sasa kubadili tabia yao. Nina matumaini kwamba watayafanyia kazi yale ambayo tumekuwa tukiwaeleza kwa miezi kadhaa,'' alisisitita Pompeo. Hata hivyo Pompeo hajaeleza wazi ni lini mazungumzo hayo ya amani yatafanyika tena.

Afghanistan Herat Taliban Kämpfer

Wapiganaji wa Taliban

Rais Trump amesitisha mazungumzo na Taliban kutokana na shambulizi katika eneo la kibalozi karibu na ubalozi mdogo wa Marekani mjini Kabul ambalo lilisababisha kifo cha mwanajeshi mmoja wa Marekani siku chache zilizopita. Katika shambulizi hilo, watu wengine 12 waliuawa.

Taliban yaacha milango wazi

Kwa upande wake kundi la Taliban limesema Marekani itaumia zaidi kuliko upande wowote ule, lakini milango iko wazi kwa ajili ya mazungumzo katika siku zijazo. Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwamba bado wanaamini Marekani watarejea tena katika meza ya mazungumzo.

''Mapambano yetu katika miaka 18 iliyopita yanapaswa kuithibitishia Marekani kwamba hatutoridhishwa hadi tutakaposhuhudia kuondoka kabisa kwa wanajeshi wote wa Marekani Afghanistan,'' alifafanua Mujahid. Taliban imesema uamuzi wa Trump utaiumiza Marekani, msimamo wao wa kupinga amani utaonekana zaidi kwa ulimwengu, watazidi kupoteza fedha na jukumu la Marekani kuingilia katika siasa za kimataifa litatengwa hata zaidi.

Taarifa hiyo ya Taliban imesema kuwa kundi hilo lilishakubaliana na Marekani, hatua iliyotarajiwa kuiruhusu Marekani kuanza kuwaondoa wanajeshi wake ili Taliban nao waweza kutekeleza ahadi ya kuhakikisha hali ya usalama na utulivu inakuwepo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pande zote mbili zimekuwa zikijiandaa kwa ajili ya mpango huo kutangazwa na kusainiwa wakati Rais Trump Jumamosi usiku alipotangaza kwamba anayafuta mazungumzo hayo ya amani.

Ujerumani yasitisha mafunzo

Wakati huo huo, polisi wa Ujerumani wamesitisha kutoa mafunzo kwa maafisa wa Afghanistan mjini Kabul kutokana na shambulizi la wiki iliyopita lililofanywa na Taliban na kuwaua kiasi ya watu 18 na wengine 100 kujeruhiwa.

Polisi 22 wa timu ya Ujerumani inayotoa mafunzo kwa maafisa wa Afghanistan, walikuwepo kwenye eneo lenye majengo ya ofisi za mashirika ya misaada pamoja na mashirika ya kimataifa mjini Kabul wakati shambulizi hilo linatokea. Polisi hao walisalimika, lakini hawawezi kuyatumia tena makaazi yao pamoja na ofisi zao.

Eine Soldatin der deutschen Feldjäger trainiert zusammen mit den deutschen Polizisten afghanische Kollegen

Askari polisi wa Ujerumani akitoa mafunzo kwa wanajeshi wa Afghanistan

Taarifa iliyotolewa mjini Berlin na msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani imeeleza kwamba kutokana na shambulizi hilo, polisi hao wa Ujerumani wamesitisha kutoa mafunzo, huku nusu ya timu ya maafisa hao wakiondolewa Afghnaistan na wengine wakipelekwa katika ubalozi wa Ujerumani mjini Kabul.

EU: Uchaguzi wa Afghanistan ni muhimu

Wakati hayo yakijiri, mjumbe maalum wa Umoja wa Ulaya nchini Afghanistan, Roland Kobia amesema uchaguzi wa urais lazima ufanyike mwezi huu kutokana na kwamba nchi hiyo inahitaji uongozi wa kisiasa wenye nguvu mpya ya kidemokrasia kutoka kwa raia wake.

Kobia ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba uchaguzi nchini humo unazidi kuwa muhimu na kudhihirika kwamba kuna haja kubwa ya uchaguzi.

Matamshi ya Kobia yametolewa saa chache baada ya Rais Trump kutangaza kuyafuta mazungumzo ya amani kati yake na Taliban. Uchaguzi wa urais umepangwa kufanyika Septemba 28, lakini kundi la Taliban linaupinga.

(AFP, AP, DPA, Reuters)