1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suala la mgogoro wa Ukrain Kubeba ajenda kuu ya mazungumzo

Admin.WagnerD25 Septemba 2015

Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Vladimir Putin wa Urusi wanatarajiwa kukutana mjini New York wiki ijayo mnamo wakati hali ya hofu ikizidi kutanda barani Ulaya na Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/1GdUr
Rais Vladimir Putin wa Urusi na Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Vladimir Putin wa Urusi na Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: Getty Images/AFP/J. Samad

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu ya Marekani mazungumzo hayo yatajikita zaidi katika mzozo wa mashariki mwa Ukraine ambako majeshi yanayoungwa mkono na Urusi yanapambana na serikali ya Ukraine hali iliyopelekea kuwepo kwa vikwazo ambavyo tayari vimeathiri kwa kiwango kikubwa uchumi wa Urusi.

Kwa upande wake Urusi imesema ya kuwa mazungumzo hayo yataangazia zaidi mgogoro wa Syria ambako Urusi imejiimarisha zaidi kijeshi katika siku za hivi karibuni kwa kupeleka ndege zake za kivita pamoja na vifaa vingine vya kijeshi.

Msemaji wa Rais Vladmir Putin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari ya kuwa mazungumzo hayo yatajikita zaidi katika suala la Syria na alipoulizwa iwapo suala la Ukraine litajadiliwa alisema itategemea kama muda utaruhusu

Viongozi hao watakuwa mjini New York kwa ajili ya kuhutubia mkutano wa baraza kuu la umoja wa mataifa jumatatu asubuhi wiki ijayo.

Msemaji wa Rais Putin alisema kikao cha viongozi hao wawili kitafanyika mara tu baada ya hotuba ya Rais Putin katika baraza hilo la umoja wa mataifa ingawa msemaji wa ikulu ya Marekani alikataa kuweka wazi siku na wakati kikao hicho kitafanyika.

Pande zote mbili pia zilionekana kutofautiana juu ya nani alietisha kikao hicho.wakati msemaji wa ikulu ya Urusi akisema kikao hicho kimeitishwa kwa makubaliano ya pamoja lakini msemaji wa ikulu ya Marekani Earnest alisema kikao hicho kimeombwa na Rais Vladmir Putin wa Urusi.

Rais Assad atakiwa kuwekwa kando katika majadiliano yanayohusu mgogoro wa Syria.

Wakati hayo yakiendela wazo la Kansela wa Ujerumani Angela Merkel la kumshirikisha Rais Bashar al-Assad katika mazungumzo yenye lengo la kutatua mgogoro wa kivita unaofukuta nchini Syria limeonekana kugonga mwamba baada ya kutoungwa mkono na Waziri wake wa mambo ya nchi za nje Frank Walter Steinmeir.

Rais wa Syria Bashar al- Assad
Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: Reuters/SANA

Kauli hiyo ya Kansela Merkel aliitoa baada ya mkutano wa viongozi wa mataifa ya umoja wa Ulaya yaliyohusu suala la wakimbizi ambao ulifanyika mjini Brussels mapema hapo jana. "Tuna paswa kuzungumza na wadau mbalimbali kuhusiana na mzozo huu" Alisema Merkel kauli ambayo ilionekana pia kuungwa mkono na Urusi.

Hata hivyo suala hilo la kuhusishwa kwa Rais Assad katika majadiliano yanayohusu mgogoro huo wa Syria limeonekana kupingwa pia na wanadiplomasia mbalimbali mjini Berlin wakidai anahusika moja kwa moja na mgogoro huo wa Syria.

Mwandishi: Isaac Gamba/DPAE/RTRE

Mhariri:Yusuf Saumu