1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi kuzungumza juu ya mgogoro wa Ukraine

Zainab Aziz Mhariri: Amina Mjahid
12 Februari 2022

Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Marekani Joe Biden watafanya mazungumzo kwa njia ya simu leo Jumamosi. Viongozi hao wanatarajiwa kuzungumzia juu ya mvutano kati ya Urusi na Ukraine.

https://p.dw.com/p/46vSr
USA Russland Kombo Joe Biden und Putin
Picha: Eric Baradat/Pavel Golovkin/AFP

Marekani imesema uwezekano wa Ukraine kuvamiwa na Urusi ni mkubwa huku ikitangaza mipango ya kuuhamisha ubalozi wake kutoka kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kiev. Kabla ya kuzungumza na Biden, rais Putin atazungumza na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye walikutana mjini Moscow mapema wiki hii kujaribu kuutatua mgogoro huo.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Adam Schultz/White House/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov ameilaumu Marekani kwa kuendeleza propaganda kuhusu uwezekano wa nchi yake kuivamia Ukraine. Lavrov aliyasema hayo wakati wa mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi katika taarifa yake juu ya mazungumzo hayo ya simu kati ya Lavrov na Blinken imesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi alimwambia mwenzake wa Marekani kwamba Umoja wa Ulaya na Marekani zimepuuza mapendekezo yaliyotolewa na Urusi kutaka ipewe uhakika juu ya usalama wake.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Mikhail Metzel/SPUTNIK/AFP

Kwingineko, nchi mbalimbali ikiwemo Ujerumani zimeendelea kuwataka raia wake kutondoka kutoka nchini Ukraine. W izara ya mambo ya nje ya Ujerumani imewashauri raia wa Ujerumani waliopo nchini Ukraine na ambao hawana sababu za lazima za kuendelea kubakia nchini humo kuondoka mara moja ikisema uvamizi wa kijeshi unaweza kutokea baada ya Marekani kuonya kwamba Urusi inaweza kuanza kuishambulia Ukraine siku yoyote. Kwa upande wake Urusi imekanusha madai hayo.

Wakati huo huo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema onyo la Marekani juu ya nchi yake kuvamiwa kijeshi na Urusi ni tamko linalozidisha hofu na ametaka utolewe ushahidi kuhusu uvamizi uliopangwa na Urusi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Ukrainian Presidential Press/AP/picture alliance

Zelensky amesema watu wa Ukraine wanaelewa kuwa kuwa hatari zipo lakini kwa sasa adui mkubwa wa wananchi ni hofu na kwamba taarifa kuhusu Ukraine kuvamiwa kijeshi zinazusha hofu na wala haziwasaidii watu wa Ukraine.

Vyanzo: AP/AFP/DPA