Maporomoko ya taka yaua 46 Ethiopia | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.03.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maporomoko ya taka yaua 46 Ethiopia

Watu 46 wameuawa na wengine wamejeruhiwa kutokana na maporomoko ya taka mjini Addis Ababa, Ethiopia. Wakaazi wa eneo hilo wanasema sababu ni ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha gesi, unaofanywa juu ya mlima wa takataka.

Tukio hilo lililotokea Jumamosi iliyopita lilisababisha nyumba kadhaa kuporomoka, karibu na jaa la takataka la Koshe pale mrundiko wa takataka pamoja na ardhi vilipoziangukia nyumba za watu kutoka sehemu ya juu.

Msemaji wa polisi katika mji wa Addis Ababa, Dagmawit Moges, amesema kuwa watu 46 wameuawa, 32 miongoni mwao ni wanawake na 12 wanaume ikiwa ni pamoja na watoto.

Wengi wa waathirika ni wasafishaji wa mji wanaoishi katika eneo hilo la jaa la taka la hekari 30.

"Tuliwaonya waache kulimbikiza takataka juu ya mlima. Nadhani uamuzi wa maafisa wa serikali wa kuanza tena kutupa takataka katika eneo hili miezi kadhaa iliyopita ndio sababu kuu ya ajali hii, ambayo hadi sasa imeshafunika nyumba zipatazo 20. Nadhani watu wapatao 150 walikuwapo katika eneo hili wakati wa maporomoko," amesema mmoja wa wakaazi wa eneo hilo Assefa Teklemahimanot.

Wapita njia wamewaambia waandishi habari kuwa bado kuna watu ambao wamefunikwa na marundo ya takataka, lakini polisi wamewazuia watu kulisogelea eneo hilo.

Jaa la zaidi ya miongo minne

Kwa zaidi ya miaka 40 jaa la Koshe limekuwa ni sehemu kuu ya kutupa takataka mjini Addis Ababa, jiji linalokuwa kwa kasi kubwa na ambalo tayari lina zaidi ya wakaazi milioni nne.

Kulingana na wakaazi wa eneo hilo, kuna takriban nyumba 50 zilizojengwa karibu na jaa hilo la takataka. Kila nyumba moja inaishi watu wapatao saba.

Äthiopien Erdrutsch (picture-alliance/AP Photo/E. Meseret)

Wakaazi wa eneo la jaa la takataka la Koshe lilokumbwa na maporomoko ya ardhi

Ibrahim Mohammed ni mkaazi wa eneo hilo ambaye nyumba yake ilinusurika chupuchupu, anasema maporomoko hayo ya ardhi yaliychukuwa dakika tatu tu. Mohammed anakadiria zaidi ya watu 500 wanaishi katika makaazi hayo.

Mkusanyaji wa takataka anayeshi katika eneo hilo hilo, Berhanu Degefe ambaye nyumba yake haikuathirika, amesema nyumba nyingi katika eneo hilo zilijengwa miaka mitatu iliyopita.

Akiwazungumzia wakaazi wa eneo hilo, Degefe amesema wanategemea kazi ya kuokota takataka kuendesha maisha yao.

Degefe amesema sababu ya maporomoko hayo ya ardhi ni kiwanda cha kuzalisha bio gesi kinachojengwa juu ya mlima huo wa takataka.

Degefe amesema wajenzi wa kiwanda hicho walikuwa wakiichimba eneo la juu na hilo liliongeza uzito juu ya mlima ambao tayari umelimbikizwa takataka na kusababisha ardhi chini yake kuporomoka.

Katika miaka ya hivi karibuni Ethiopia imekuwa moja wapo ya nchi za Afrika inayoimarika kiuchumi kwa kuvutia wawekezaji wa kigeni, lakini bado kuna zaidi ya watu milioni 20 wanaoishi katika hali duni ya umasikini.

Wakosoaji wanasema tatizo ni sera za kiuchumi za serikali ambazo haziwalengi raia masikini walio wengi.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/dpa

Mhariri: Gakuba, Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com