Mapinduzi ya Mauritania yalaaniwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mapinduzi ya Mauritania yalaaniwa

Jumuia ya kimataifa yadai katiba iheshimiwe nchini Mauritania

default

Wanajeshi wanapiga doria mjini Nouakchott


Viongozi wa kijeshi waliempindua rais aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasi nchini Mauritania wanasaka uungaji mkono wa raia na kujaribu kuituliza jumuia ya kimataifa inayolaani mapinduzi hayo.


Mamia ya watu waliopanda magari na wengine kwenda kwa miguu wameandamana leo mchana mjini Nouakchott kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na mkuu wa zamani wa vikosi vya ulinzi wa rais,jenerali Mohammed Ould Abdel Aziz.


Kwengineko nchini humo wananchi wameendelea kama kawaida na pirika pirika zao za kimaisha, huku magari ya polisi waliovalia kivita yakipiga doria na kulinda vituo muhimu.


Jana usiku baraza la majenerali watatu na makanali wanane wakiongozwa na jenerali Ould Abdel Aziz,limetangaza "mwisho wa madaraka ya rais Sidi Ould Cheikh Abdallahi,aliyechaguliwa katika uchaguzi huru mwezi March mwaka jana na kuahidi kuitisha  uchaguzi "huru na wa uwazi" mnamo muda mfupi ujao.""Nnaahidi kudhamini binafsi kanuni za dola linaloheshimu sheria,uhuru wa raia na taasisi za kidemokrasi " amesema kiongozi huyo mpya wa Mauritania mwenye umri wa miaka 52.


Uongozi wa kijeshi umeahidi pia kuheshimu makubaliano yote ya kimataifa yaliyotiwa saini na Mauritania.


Wanamapinduzi wanaonyesha kutaka kuituliza jumuia ya kimataifa inayolaani mapinduzi hayo, yaliyojiri miezi 15 tuu baada ya uchaguzi wa rais uliosifiwa kama "mfano wa kuigizwa barani Afrika na katika ulimwengu wa kiarabu kwa jumla."


Misri imesema hii leo imefadhaishwa na mapinduzi hayo huku jumuia ya nchi za kiarabu ikisema imeingiwa na wasi wasi na Ufaransa ikitishia kutathmini upya uhusiano wa umoja wa Ulaya na Mauritania ikiwa katiba haitaheshimiwa.


Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon,Umoja wa Afrika,halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya,Marekani na jumuia ya nchi za kiislam,wote hao wamelaani mapinduzi ya Mauritania.


Rais Umaru Yaradua wa Nigeria anasema:


"Nigeria haitaitambua na inalaani aina yoyote ya mageuzi ya serikali ambayo hayajafanyika kuambatana na katiba.Nigeria kwa hivyo inalaani yaliyotokea Mauritania."


Ufaransa ambayo ndio mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya,imewataka viongozi wa kijeshi wawaachie huru haraka,rais,waziri mkuu na mawaziri wote wanaoshikiliwa.

Nchini Mauritania kwenyewe "vita vya maneno" vimeripuka kupitia vyombo tofauti vya habari, kati ya wasemaji wawili wa serikali.


Kwa upande mmoja,Abdullaye Mahmadou Ba (anaesema ameingia mafichoni ili asikamatwe,)ameitolea mwito jumuia ya kimataifa "isiutambue utawala wa kimapinduzi na wasikubali kudanganywa na kiini macho cha uchaguzi."


Kwa upande wapili,mbunge Sidi Mohammed Ould Maha akizungumza kwa niaba ya wabunge waliojitenga na chama tawala wiki iliyopita,amewatolea mwito wananchi washiriki katika maandamano kuwaunga mkono wanajeshi. • Tarehe 07.08.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EsOt
 • Tarehe 07.08.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EsOt
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com