Mapinduzi ya kidemokrasia yasonga mbele Uarabuni | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mapinduzi ya kidemokrasia yasonga mbele Uarabuni

Nchi za magharibi zinazungumzia sana juu ya maadili yao, lakini harakati za kupigania demokrasia katika nchi za Kiarabu hivi sasa, zinaonyesha, kwa uwazi wote, pengo kubwa lililopo kati ya matakwa na hali halisi.

Waasi wa Libya wakirudi nyuma baada ya kushambuliwa

Waasi wa Libya wakirudi nyuma baada ya kushambuliwa

Siyo zaidi ya maneno ya vidokezo, wakati wanasiasa wa nchi za Magharibi wanapozungumzia juu ya maadili ya uhuru na demokrasia na juu ya ulazima wa kuyatetea maadili hayo.

Lakini wakati wale wanaoishi katika jamii za maonevu wanapojaribu kuondokana na jamii hizo, watu hao hawawezi kuwa na matumaini kwamba wanasiasa wa nchi za magharibi watayatekeleza hayo wanayoyasema.

Ni vigumu kuelezeka kwa nini wanasiasaa hao hao, wa Magharibi wapo tayari kwenda vitani dhidi ya madikteta fulani- kwa mfano Saddam Hussein wa Irak, lakini, wakati huo huo, wanashirikiana na madikteta wengine kwa undani, kama vile walivyofanya na aliekuwa Rais wa Tunisia, Zine Al-Abidine Ben Ali.

Ni wazi kwamba pana sheria za kimataifa zinazoweka msingi wa ruhusa na mipaka ya kujiingiza katika mambo ya nchi nyingine, lakini sheria hizo zinawekwa kando kwa urahisi panapohusu hali fulani. Kwa mfano sasa hali ya Libya.

Rais Barack Obama wa Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani

Marekani, ambayo wakati wote inatuhumiwa katika hali kama hizo, sasa haiwezi kutuhumiwa. Rais Barack Obama alikuwa anasitasita, na ameingizwa katika vita na Ufaransa, yumkini baada ya kujaribu kusahau ukaribu wa muda mrefu baina ya Rais Sarkozy na Kanali Gaddafi.

Mjini Washington na katika miji mingine mikubwa, baadhi wanawashukuru Wamisiri na Watunisia kwamba wamefanya mapinduzi wao wenyewe bila ya msaada kutoka nje; maana ikiwa wangeliwaruhusu watu wa nje wawafanyie mapinduzi haya, basi haraka sana wangelijikuta chini ya watawala wengine!

Lakini mazingira ya nchini Libya ni tofauti kabisa, kwa sababu upinzani ni dhaifu na utajiri wa mafuta ni mkubwa.

Wahusika wanahoji kwamba siyo sahihi kuwasaidia wapinzani ili washinde katika mapinduzi yao, kwa sababu huo utakuwa uingiliaji kati wa moja kwa moja. Lakini wakati huo huo hakuna anayetaka kuyasamehe mafuta ya Libya! Na ndiyo sababu pametokea hoja za kutetea hatua za kijeshi zenye shabaha za kibinadamu.

Maandamano ya kuwaunga mkono Wabahrain, nchini Iraq

Maandamano ya kuwaunga mkono Wabahrain, nchini Iraq

Katika Saudi Arabia, Bahrain na katika nchi nyingine za Kiarabu, maslahi ya mafuta na ya kiuchumi yanawekwa mbele, sambamba na jinsi mvutano na Iran unavyotumiwa. Maslahi hayo ni muhimu kuliko sera ya kuziunga mkono harakati za kuleta demokrasia.

Na nchini Yemen maslahi yapo katika mchango unaotolewa na Rais wa nchi hiyo, Ali Abdullah Saleh, katika harakati za kuwakabili magaidi wa Al-Qaida. Kwa hiyo, siyo sahihi kumdhoofisha mtu kama huyo.

Lakini ikiwa nchi za Magharibi zinachelewa kuchukua hatua, patakuwa na hatari ya watu kuzipa kisogo nchi hizo baada ya kufanikiwa katika harakati za kupigania uhuru wao.

Mapinduzi hayo yanaweza kuchelewa kufanikiwa katika sehemu fulani, lakini mchakato huo hautarudi nyuma. Baada ya kujikomboa kuondokana na ukoloni, sasa unafuatia ukombozi wa kuondokana na udhalimu wa ndani.

Mwandishi: Peter Philipp/ZR
Tafisri: Mtullya, Abdu
Mhariri: Miraji Othman

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com