1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yastishwa Somalia

27 Aprili 2007

Mamia ya wenyeji wa Somalia wameanza kurudi Mogadishu baada ya serikali ya mpito kutangaza kuwa imeyashinda makundi ya waasi waliokuwa wakizusha ghasia mjini Mogadishu. Ghasia hizo zilizoendelea kwa siku tisa mfululizo zilisababisha vifio vya watu mia nne na laki nne kutorokea nchi jirani.

https://p.dw.com/p/CHFK
Wanajeshi wa Hawiye wafyatulia risasi wanajeshi ya Ethiopia.
Wanajeshi wa Hawiye wafyatulia risasi wanajeshi ya Ethiopia.Picha: AP

Muda tuu waziri mkuu Mohammed Ali Ghedi alipotangaza kuwa, kwa ushirikiano na wanajeshi wa Ethiopia waliyafurusha makundi ya waasi,risasi zilifyatuliwa katika hoteli moja mjini Mogadishu.

Watu hao waliokuwa wamejifinika nyuso zao waliishambulia hoteli hiyo na kufyatua risasi kwa saa moja mfululizo,na kuibua swali ikiwa amani hii iliyotangazwa hivi punde itadumu.

Siku tisa zilizopita zimekuwa za dhiki kubwa kwa wenyeji wa Somalia pamoja maafisa wa mashirika ya kiutu. Zaidi ya watu laki nne walilazimika kukimbilia hifadhi kwenye maeneo yaliokuwa na utulivu. Mapigano hayo baina ya wanamgambo wa mahakama za kiislamu,jamii ya wahawiye na wanajeshi wa Somalia na Ethiopia yalikuwa mbaya kiasi cha kwamba ilibidi wakimbizi hao kulipia kodi sehemu zilizokuwa na utulivu.

Wengi walilazimika kununua nafasi hata kukaa juu ya miti kutokana na msongamano wa watu.

Mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Mogadishu John Holmes, aliambia waandishi habari kuwa imekuwa vigumu kwao kutoa misaada kwa raia.

Hivi majuzi Mjumbe wa Mareknai nchini Kenya Michael Rannenberger na Mratibu wa maswala ya kiutu wa Umoja wa mataifa Graham farmer walimwandikia waziri mkuu wa Somalia Mohammed Ghedi kushtumu visa vya maafisa wao kuzuiwa na kushurutishwa kutoa hongo katika vitu vya ngede mjini Mogadishu.

Lakini waziri mkuu Mohammed Ghedi alisema hakuna uwezekano wa hata mashirika ya kiutu kuendesha shughuli zao bila kupitia vizuizi. Hali ni tete nchini humo na usalama lazima udhibitiwe kwa njia yeyote ile.

Wanajeshi wa Ethiopia wakishirikiana na wale wa Somalia wameendelea kushika doria katika maeneo yote Mogadishu na kupekuwa kila gari nyumba na watu wanaoshukiwa kuwa waasi. Lakini mwenyeji mmoja wa Kaskazini Mogadishu Ibrahim Sheik Mao alisema kuwa ``wamekamata mamia ya watu hata wale wasio na hatia na ndio sababu wengi wetu tunatoroka´´.

Lakini licha ya juhudi hizi za wanajeshi nchini Somalia kudhibiti mapigano hayo ambayo yamekuwa mabaya zaidi katika miaka 15 ya vita nchini humo, mabalozi wanahofia kuwa huenda mapigano yakazuka tena,kwani wanajeshi waliopo Mogadishu hawatoshi kupambana na makundi ya waasi yanayojitokeza kila wakati.

Isabella Mwagodi