Mapigano yasitishwa mashariki mwa Ghouta huku Umoja wa Mataifa ukitaka Syria ifikishwe ICC | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mapigano yasitishwa mashariki mwa Ghouta huku Umoja wa Mataifa ukitaka Syria ifikishwe ICC

Usitishaji mapigano mashariki mwa Ghouta umeanza kutekelezwa kwa sharti la kuruhusu uingizaji wa misaada ya kiutu. Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuitaka Syria kushitakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Usitishaji mapigano katika mji wa mashariki wa Ghouta ulianza usiku (Ijumaa) baada ya Urusi kusimamia makubaliano yaliyofikiwa kati ya waasi na vikosi vya Syria.

Msemaji mkuu wa muungano wa makundi ya upinzani ya nchini Syria (SNC), Ahmad Ramadan, amesema, "Makubaliano ya kutekeleza usitishaji wa mapigano mashariki mwa mji wa Ghouta yalifikiwa Ijumaa."

Rami Abdel Rahman, mkuu wa shirika linalofuatilia ukiukaji wa haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza amesema, "Waasi katika eneo hilo wameweka sharti kuwa misaada ya kiutu inapaswa kufika katika eneo hilo ndani ya saa 48 zijazo vinginevyo makubaliano ya kusitisha mapigano yatafutwa." 

Mashariki mwa Ghouta kumezingirwa kwa kipindi cha miaka minne huku watu wapatao 393,000 wakiwa hawawezi kupatiwa misaada ya kiutu.

Jumatano Urusi ilikana madai ya kwamba kwa ushirikiano na jeshi la serikali ya Syria inahusika na shambulio la kemikali mashariki mwa Ghouta lililotokea Januari 22.

Schweiz UN Friedensgespräche für Syrien (picture-alliance/Photoshot/Xu Jinquan)

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura

Wito wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua ya mahakama dhidi ya Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa mara nyingine ametoa wito kwa Syria kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa "ukiukaji mkubwa" katika kuzuia misaada ya kiutu na huduma za matibabu.

Guterres amesema kwamba mnamo mwezi Desemba hakuna misaada ya kiutu iliyofikiswa kwa zaidi ya watu 417,000 katika maeneo tisa yaliyozingirwa. Ni watu 60,000 kati ya Wasyria milioni 2.5 walio katika maeneo 'yaliyo vigumu kufikiwa'  waliopokea misaada ya kiutu, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema katika ripoti yake kuhusu hali ya kibinaadamu nchini Syria iliyowasiliswa Ijumaa katika Baraza la Usalama.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema " uwezo wa Umoja wa Mataifa pamoja na washirika wake kuwafikia watu wanaoishi katika maeneo yaliyozingirwa na yaliyo vigumu kufikiwa bado ni suala muhimu sana." Alilichagua eneo la mashariki mwa Ghouta ambako bei za bidhaa za msingi zimepanda na kuwa mara 30 zaidi ikilinganishwa na mji jirani wa Damascus, "bei zinazopindukia uwezo wa wakaazi wengi."

Guterres amezitolea wito nchi zenye ushawishi katika serikali ya Syria na wapiganaji wa upinzani kuwezesha uhamishaji wa watu wanaohitaji matibabu pamoja na ufikishaji wa misaada ya kiutu. Maafisa wa Syria wameendelea kuondoa "vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha na vifaa vya afya" kutoka katika misafara ya mwezi uliopita, alisema.

Lakini wito mwengine wa kutaka kuishitaki serikali ya Syria katika mahakama ya ICC hauna uwezekano wa kufanikiwa. Urusi na China zilipinga kwa kura ya turufu azimio la Baraza la Usalama lililoungwa mkono na nchi 60 mwezi Mei 2014 la kulifikisha suala la mgogoro wa Syria katika mahakama ya kimataifa.

Upinzani kususia mazungumzo ya Sochi

Baada ya siku mbili za mazungumzo mjini Vienna pamoja na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura, Kamati Kuu ya Majadiliano (HNC) ya upinzani wa Syria imesema hatitohudhuria mkutano wa amani utakaosimamiwa na Urusi wiki ijayo.

"Kamati ya HNC imetangaza kususia mkutano wa Sochi ambao Urusi imeialika," imeandika kwenye akaunti yake ya Twitter kwa lugha ya Kiarabu siku ya Ijumaa.

Schweiz Syrische Opposition bei Friedensgesprächen in Genf (Getty Images/AFP/F. Coffrini)

Kamati Kuu ya Majadiliano ya upinzani wa Syria (HNC)

Urusi imeripotiwa kutuma mialiko ipatayo 1,600 kuhusu "kikao chake cha amani" cha siku mbili katika hoteli ya mapumziko ya mjini Sochi karibu na Bahari Nyeusi wiki ijayo, kujadili suala la katiba ya Syria.

Msemaji mkuu wa upinzani wa Syria katika mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa mjini Vienna, Yahya al-Aridi amesema mazungumzo ya Sochi ni njama za kuvuruga juhudi za Umoja wa Mtaifa za mazunguzmo ya amani: "Duru hii ya mazungumzo ya Vienna ilikuwa muhimu sana, lilikuwa ni jaribio la uwajibikaji. Na hutakuona uwajibikaji wowote. Na Umoja wa Mataifa nao haujaona uwajibikaji wowote."

De Mistura alieleza kwamba Urusi imesema mazungumzo ya Sochi yana lengo la kuunga mkono mchakato wa Umoja wa Mataifa, "Taarifa ya Shirikisho la Urusi imesema kuwa matokeo ya kikao cha (Sochi) yatawasilishwa mjini Geneva kama mchango katika mchakato wa mazungumzo ya Syria yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa. "

 

Mwandishi: Yusra Buwayhid/DW/

Mhariri: Isaac Gamba

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com