1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yapamba moto Ukraine

27 Mei 2014

Vikosi vya Ukraine vimepambana na waasi wanaotaka kujitenga katika mji wa Donetsk kwa siku ya pili baada ya kuwaingiza katika hasara kubwa waasi hao na serikali imeapa kutokomeza magaidi wote nchini humo.

https://p.dw.com/p/1C7mq
Wapiganaji waasi wakiwasili karibu na uwanja wa ndege wa Donetsk.(26.05.2014)
Wapiganaji waasi wakiwasili karibu na uwanja wa ndege wa Donetsk.(26.05.2014)Picha: picture-alliance/AP

Waasi wanasema zaidi ya wapiganaji wao hamsini wameuwawa.Meya wa Donetsk ambacho ni kitovu cha viwanda cha wakaazi milioni moja mashariki mwa Ukraine anasema idadi ya vifo kutokana na mapigano hayo yaliyozuka jana Jumatatu imefikia 48 wakiwemo raia wawili.

Muandishi wa shirika la habari la Uingereza Reuters amehesabu miili 20 yenye sare za kijeshi ikiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti hospitalini baadhi ya miili hiyo ikiwa haina viungo fulani vya mwili.Waasi wanasema wote hao wameuwawa wakiwa kwenye gari la kijeshi ambalo lilikuja kushambuliwa vikali na jeshi.

Operesheni ya kijeshi Donetsk

Ukraine ilianzisha mashambulizi mapya dhidi ya waasi ambao walikuwa wakikalia vituo muhimu katika mji wa Donetsk na miji mengine mashariki mwa nchi hiyo muda mfupi baada ya uchaguzi wa rais wa Jumapili. Mshindi wa uchaguzi huo Petro Poroshenko amekataa mazungumzo yoyote yale na waasi hao aliowaita "magaidi".

Mpiganaji muasi akiwa ndani ya jengo la uwanja wa ndege wa Donetsk. (26.5.2014)
Mpiganaji muasi akiwa ndani ya jengo la uwanja wa ndege wa Donetsk. (26.5.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Serikali ya Ukraine leo imeishutumu Urusi kwa kutuma magaidi kuingia nchini Ukraine baada ya walinzi wa mipakani kupambana na watu wenye silaha mashariki ya Ukraine wakati wa usiku. Urusi imerudia tena wito wake wa kuitaka Ukraine kusitisha operesheni zake hizo za kijeshi.

Ukraine imefanya mashambulizi ya anga na ya ardhini hapo jana kuwatimuwa waasi kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Donetsk na kufanikiwa kuwatowa kwenye jengo la uwanja huo ilipofika usiku.Hivi sasa vikosi vya Ukraine ndio vyenye kuudhibiti uwanja huo.

Lakini mapigano yaliendelea usiku kucha hadi leo asubuhi ambapo barabara ya kuelekea uwanja wa ndege ilikuwa na ishara za kuwepo kwa mapigano ya usiku na milio mizito ya bunduki iliweza kusikika kutoka masafa ya mbali asubuhi hii.

Hasara kubwa kwa waasi

Waziri wa mambo ya ndani Arsen Avakov amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kiev kwamba uwanja wa ndege huo uko chini ya udhibiti wao kikamilifu na kwamba maadui wamepata hasara kubwa bila ya wao kuhasirika.

Helikopta ikifyatuwa mizinga dhidi ya waasi walioko kwenye jengo la uwanja wa ndege wa Donetsk.(26.05.2014)
Helikopta ikifyatuwa mizinga dhidi ya waasi walioko kwenye jengo la uwanja wa ndege wa Donetsk.(26.05.2014)Picha: Reuters

Naibu wa kwanza wa waziri mkuu Vitaly Yarema amesema pembezoni mwa mkutano mmoja wa serikali kwamba wataendelea na operesheni ya kupambana na ugaidi hadi hapo patakapokuwa hakuna gaidi anayebakia kwenye ardhi ya Ukraine.

Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE) limesema limepoteza mawasiliano na timu yake moja ya waangalizi katika eneo la Donetsk. Timu hiyo inayomjumuisha raia mmoja wa Estonia, Mswisi,Mturuki na Mdanish ilikutana jana usiku katika kituo kimoja cha ukaguzi barabarani na tokea wakati huo haikuweza kurudisha mawasiliano.

Mwandishi :Mohamed Dahman/Reuters

Mwandishi: Josephat Charo