Mapigano yapamba moto Damascus | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mapigano yapamba moto Damascus

Vikosi vya serikali ya Syria vimeendelea kuhujumu kwa mabomu vitongoji vya mji mkuu Damascus vinavyodhibitiwa na waasi,vikizidisha kishindo katika mitaa inayosemekana ilihujumiwa kwa silaha za kemikali.

Wanajeshi wa Syria wazungumza na mwandishi habari waalipokuwa wakipiga doria katika kitongoji cha mji mkuu- Jobar.

Wanajeshi wa Syria wazungumza na mwandishi habari waalipokuwa wakipiga doria katika kitongoji cha mji mkuu- Jobar.

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa lilikutana kwa dharura jana jioni na kuhimiza uchunguzi ufanywe kuhusu kutumiwa silaha za kemikali katika vitongoji vya mji mkuu wa Syria,lakini wajumbe mkutanoni hawakuafikiana kama wachunguzi wa Umoja wa Mataifa ambao tayari wako Damascus wachunguze tuhuma hizo au la.

Marekani,Ufaransa na Uingereza pamoja na kundi la mataifa zaidi ya 30 mengine yalimtaka mkuu wa tume ya Umoja wa mataifa nchini Syria,Ake Sellstrom wa Sweeden,aliyewasili pamoja na kundi lake jumapili iliyopita mjini Damascus kuchunguza madai ya kutumiwa silaha za kemikali katika mzozo wa Syria,achunguze pia tuhuma hizi mpya haraka iwezekanavyo.

Madai kama hayo yametolewa pia na upande wa upinzani nchini Syria.Mwanaharakati mmoja amesema:

"Wanawataka wachunguzi waje na wawaone watu waliouliwa katika kitongoji cha Damascus, wawaone wahanga,na wachunguze nani ametumia silaha za kemikali."

Laurent Fabius ataka jibu la nguvu la kimataifa

Ingawa baraza la usalama halikuunga mkono fikra hiyo kutokana,kama wasemavyo wanadiplomasia,upinzani wa Urusi na China,hata hivyo wanachama 15 wa baraza hilo wamesifu wito wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon kutaka ukweli wa mambo ufichuliwe.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema hivi punde "angependelea jibu la nguvu kutoka jumuia ya kimataifa" ikiwa ushahidi utapatikana kwamba serikali ya Syria imetumia silaha za kemikali." Akihojiwa na vituo vya televisheni vya Ufaransa, Waziri Fabius amesema "hakuna haja ya kutumwa wanajeshi na kuongeza" Ikiwa baraza la usaalama litashindwa kupitisha uamuzi,utabidi upitishwe kwa njia nyengine". Hakutaja lakini njia gani.

Waziri mwenzake wa Ujerumani Guido Westerwelle ametoa wito wachunguzi wa Umoja wa mataifa walioko mjini Damascus waruhusiwe haraka kuingia na kuchunguza madai hayo.

Iran,mshirika wa serikali ya mjini damascas inahisi Serikali ya Syria haiwezi kutwikwa dhamana ya shambulio la kemikali na kama shambulio hilo kweli limetokea basi,wakulaumiwa si wengine isipokuwa "makundi ya kigaidi."

Hujuma za jeshi la serikali zaendelea

Wakati huo huo vikosi vya anga na wanajeshi wa Syria wameendelea kuhujumu maeneo yanayodhibitiwa na waasi karibu na Damascus,ikiwa ni pamoja na yale maeneo ambayo upande wa upinzani unadai vikosi vya serikali vimetumia silaha za kemikali.Madege ya kivita yamehujumu mitaa ya Khan al Cheikh na Zamalka na kuwajeruhi watu kadhaa huku mapigano makali yakiendelea katika maeneo hayo" limesema shirika linalochunguza masuala ya haki za binaadam lenye makao yake nchini Uingereza.

Mitaa ya Kaboun na kambi ya wakimbizi wa kipalastina huko Yarmouk,nayo pia imehujumiwa.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com