Mapigano ya kikabila yauwa 6 Nigeria | Matukio ya Afrika | DW | 19.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mapigano ya kikabila yauwa 6 Nigeria

Kiasi cha watu sita wameuwawa katika mapigano ya kikabila mwishoni mwa juma kati ya wafugaji na wakulima katika eneo la kati nchini Nigeria, huku mamia ya raia wakiyahama makaazi yao kukimbia mapigano hayo. 

Polisi ya Nigeria imeliambia shirika la habari la AFP kwamba ghasia hizo zilizuka siku ya Jumamosi baada ya mwili wa mfugaji mmoja aliyekuwa ameporwa pikipiki yake kupatikana katika kijiji cha mashariki mwa jimbo la Taraba. 

Kamishna Polisi wa jimbo hilo, Yunana Yakubu Babas, amesema ghasia hizo zimewalazimisha mamia ya wanakijiji kukimbia makaazi yao. 

Ndugu wa mtu  huyo aliyeuwawa waliishambulia jamii ya wakulima kwa bunduki kila mtu waliyemtuhumu kufanya mauaji.

Wafugaji wa kabila la Fulani waliwashutumu watu wa kabila la Tiv, ambao ni jamii ya wakulima, kufanya uporaji na kusababisha kuuwawa watu kadhaa na mali kupotea. 

Ghasia na mauaji kati ya jamii za wafugaji na wakulima ni kitu kinachotokea mara kwa mara nchini Nigeria, hususan eneo la kati nchini humo ambako mapambano kuhusiana na malisho na haki ya kupata maji kati ya Wafulani wafugaji na wakulima vimesababisha mauaji ya watu kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.