1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano Somalia bado yanaendelea.

Sekione Kitojo23 Aprili 2007

Mapigano makali yameutikisa tena mji mkuu wa Somalia Mogadishu leo Jumatatu wakati majeshi ya Ethiopia yakiongeza mashambulizi yake dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu kwa muda wa siku ya sita leo, huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa idadi ya vifo kwa raia.

https://p.dw.com/p/CHFi
Mwanamke wa Kisomali akipita katika eneo lililoharibiwa kwa makombora mjini Mogadishu.
Mwanamke wa Kisomali akipita katika eneo lililoharibiwa kwa makombora mjini Mogadishu.Picha: picture-alliance/ dpa

Baada ya usiku wa mapigano ya hapa na pale, milipuko mikubwa ilisikika katika wilaya ya kaskazini mjini Mogadishu, mahali ambako majeshi ya Ethiopia yakiwa na vifaru na magari ya kivita yaliwashambulia wapiganaji kwa nia ya kuwaondosha kabisa katika mji huo mkuu ulioko katika pwani ya Somalia.

Kuna taarifa ya idadi kubwa ya vifo vya raia huku maeneo ya mapambano yakiwa hayaingiliki.

Nimeona vifaru vya majeshi ya Ethiopia vikiwa katika maeneo ambapo vilishambulia maeneo ya wapiganaji wa Kiislamu, amesema Mukhtar Mohammed , mkaazi wa kitongoji cha Fagar kaskazini ya Mogadishu.

Mapigano yamekuwa makubwa kuliko jana , makundi hayo hasimu yanapambana kwa bunduki, makombora pamoja na makombora ya kuangushia ndege, ameongeza.

Raia kadha walikwama katika eneo hilo la mapigano wakati miili kadha ya watu ikiwa inaoza ilikuwa imetapakaa katika majengo ambayo yameharibiwa pamoja na mitaa ambako vifaru vya Ethiopia na magari ya wapiganaji yalikuwa yakienda mbio yakiwa na wapiganaji huku wakifyatua risasi hovyo.

Mapigano hayo , ambayo yalianza siku ya Jumatano , hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 219 wengi wao wakiwa raia na kuwajeruhi wengine kadha , kwa mujibu wa shirika la amani na haki za binadamu la Elman ambalo linaangalia idadi ya watu walioathirika. Mamia ya raia, wakiwa wamebeba mali zao , walitumia nafasi ya kuwa upande wa kusini kuna hali ya utulivu na kukimbilia huko, ikiwa ni sehemu ya wimbi linalozidi kuongezeka la wakimbizi kutoka mji wa Mogadishu ambao umekumbwa na mapigano makubwa tangu kuondolewa madarakani kwa dikteta Mohammed Siad Barre.

Tunakimbia kwasababu hakuna matumaini ya kuishi katika mji huu. Tunahofu kuwa mapigano yanaendelea kuwa mabaya kila siku, amesema Hassan Mohammed, mkaazi wa eneo la Waberi kusini mwa Mogadishu.

Hatuna sehemu ambayo tunaweza kuishi katika mji huu. Kila mahali mjini Mogadishu ni sawa tu. Vifo. Tunakimbia hadi pale tutakapopata mahali ambapo ni salama , ameeleza Saadia Bur Dheere, mama wa watoto watatu, wakati akipanda gari dogo la pick up.

Jana Jumapili waziri mkuu anayeungwa mkono na majeshi ya Ethiopia Ali Mohammed Gedi aliapa kupambana na wapiganaji, baadhi wakiwa wanatuhumiwa kuwa na mahusiano na kundi la kigaidi la Al Qaeda linaloongozwa na Osama bin Laden. Hadi pale magaidi watakapoondolewa kabisa kutoka Somalia , mapigano bado yataendelea, Mohammed Gedi ameiambia radio ya Shebele mjini Mogadishu.