1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano mapya yaripotiwa mjini Jerusalem

Amina Mjahid
22 Aprili 2022

Watu kadhaa wamejeruhiwa kufuatia makabiliano mapya kati ya Wapalestina na wanajeshi wa Isarel katika eneo takatifu linalozozaniwa ndani ya mji mkongwe wa Jerusalem.

https://p.dw.com/p/4AHso
Israelische Angriffe im Gazastreifen
Picha: Yousef Masoud/AP Photo/picture alliance

Polisi nchini Israel waliuvamia uwanja wa msikiti wa Al Aqsa na kurusha mabomu ya kutoa machozi pamoja na risasi za mpira kwa vijana wa kipalestina waliokuwa wanawarushia mawe hii ikiwa ni kulingana na mpiga picha wa shirika la habari la AFP aliyekuwa katika eneo la tukio.

Makabiliano hayo yanakuja mwezi mmoja baada ya mapigano mabaya kushuhudiwa katika eneo hilo wakati wa sherehe ya wayahudi ya Passover inayokwenda sambamba na mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa waumini wa kiislamu.

Polisi imesema mapema leo alfajiri vijana hao wa kipalestina walianza kurusha mawe katika ukuta unaochukuliwa kuwa muhimu kwa waumini wa kiyahudi wanaofanya ibada zao katika eneo hilo.

Jeshi la Israel ladaiwa kutekeleza mauaji Ukingo wa Magharibi

Eneo la msikiti wa Al Aqsa ndio kitovu cha vurugu kati ya waumini wa dini ya Kiislamu na ya Kiyahudi. Msikiti huu ni eneo muhimu la tatu lililotakatifu kwa waumini wa kiislamu na  ni eneo takatifu zaidi kwa Wayahudi.

Umoja wa Mataifa umepaza sauti yake juu ya mapigano hayo na kusema ina wasiwasi ya hali inavyoendelea kuwa mbaya mjini Jerusalem. 

Zaidi ya watu 30 wajeruhiwa

Israel | Zusammenstöße auf dem Tempelberg in Jerusalem
Polisi wa Israel wakikabiliana na vijana wa kipalestina mjini JerusalemPicha: Mahmoud Illean/AP Photo/picture alliance

Shirika la hilali nyekundu limesema Wapalestina 31 wamejeruhiwa huku wengine wawili wakiwa katika hali mahututi. Ghasia hizo zimesababisha hofu ya kutokea mapigano makubwa zaidi mwaka mmoja baada ya makabiliano sawa na ya leo kutokea kwa siku kumi na moja mjini Jerusalem.

Wiki iliyopita  zaidi ya watu 200 wengi kutoka Palestina walijeruhiwa katika mapigano  kwenye uwanja wa masikiti wa Al Aqsa mjini humo.

Israel yashambulia kwa ndege za kivita Kusini mwa Gaza

Hii imesababisha mgongano zaidi wakati makundi ya wapalestina walio na silaha waliporusha maroketi yaliyoelekezwa nchini Israel kutoka ukanda wa Gaza, Israel nayo ikajibu kwa mashambulio ya angani katika ukanda huo uliozingirwa na ulio na idadi ya watu milioni 2.3

Chanzo: afp/dpa