Mapigano makali yaendelea Brega | Matukio ya Afrika | DW | 18.07.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Mapigano makali yaendelea Brega

Mapigano katika mji wenye hazina ya mafuta wa Brega nchini Libya yametoka katika eneo la jangwa na kuingia katika makazi ya watu, wakati ambapo kiongozi mkongwe wa nchi hiyo, Gaddafi akishikilia kwamba hatojiuzulu.

default

Waasi wakiwa eneo la Nafusa

Waasi wamekwishaingia katika mji wa Brega, jambo ambalo linawaweka katika nafasi ya ushindi mkubwa. Lakini, hata hivyo, bado hawajafanikiwa kuudhibiti mji wote kutoka kwa vikosi vya Gaddafi, ambavyo vimekuwa vikiushikilia mji huo tangu Aprili.

Jana jioni msemaji wa vikosi vya waasi, Mohammed Zawi, alithibitisha kufikiwa kwa hatua hiyo kwa kusema baadhi ya vikundi vyao vimefanikiwa kuingia katika mji huo, lakini, hata hivyo, bado hawajafanikiwa kuudhibiti wote.

Zawi amekanusha minong'ono iliyoeleza kwamba vikosi vya Gaddafi vimeutelekeza mji huo kwa kusema kwamba hivi sasa wanakabiliana vikali na vikosi vya Gaddafi, akifafanua kuwa hiyo ni awamu ya nne ya kampeni yao.

Hata hivyo, Shirika la Habari la Ufaransa -AFP- limesema imekuwa vigumu kuthibitisha kauli ya msemaji huyo wa waasi kwa kuwa waandishi wa habari wamezuiwa kufika katika eneo la mapigano.

Mpaka sasa mizinga mikubwa ilikuwa inatumiwa, lakini kutokana na mapigano hayo kuwa ya karibu zaidi katika maeneo ya mitaani, bunduki za rasharasha zimechukua nafasi.

Kwa mujibu wa watoa, matibabu jana wapiganaji waasi watatu waliuwawa na waasi 96 kujeruhiwa, tukio hilo linafanya idadi ya wapiganaji waliouwawa katika eneo la Brega tangu kuanza kwa mapigano hayo alhamisi iliyopita kufikia 15 na waliojeruhiwa 274.

Taarifa za NATO kutoka Brussel zinasema wanafuatilia kwa kina hali tete nchini Libya ikijumuisha eneo la Brega.

Brega ni mji uliyoundwa na maeneo matatu, makazi ya watu upande wa mashariki, sehemu yenye mafuta kwa magharibi na katikati kukiwa na mji wa zamani.

Libyen Machthaber Muammar Gaddafi in Tripolis

Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi

Katika oporesheni yake iliyofanyika leo hii mjini Brega, Jumuiya ya Kujihami ya NATO imeripotiwa kuyaripua magari manane ya silaha. Hapo jana mfululizo wa miripuko kiasi ya 13 ilisikia mjini Tripoli baada ya Gaddafi kusikia akisema hatokwenda uhamishoni.

Akisikia kwa sauti kubwa kupitia vipaza sauti, mbele ya wafuasi wake huko magharibi mwa Tripoli, mji wa Zawiyah, Gaddafi alisema kumtaka yeye aondoke ni kichekesho.

"Wanasema nitakimbilia Honolulu. hicho ni kichekesho. Je niiache nchi yangu ya mababu wetu! Niwatelekeze watu wangu! Watu wapo tayari kufa kwa niaba yangu, na mimi nipo tayari kujitoa mhanga. Nitakuwa mtu wa kwanza katika safu ya mbele ya mapambano" alisema Gaddafi.

Katika hatua nyingine, huko kusini magharibi mwa Tripoli, vikosi vya waasi vimekabiliana vikali na majeshi ya Gaddafi. Waasi na wanajeshi hao wamekabiliana na maroketi na bunduki za rasharasha.

Kwa mujibu wa shirikala habari la AFP, mapigano hayo yametokea katika milima ya Nafusa na eneo la Bir Ayad ambalo ni makutano muhimu ya barabara kubwa ya kuelekea Tripoli.

Mwandishi: Sudi Mnette/AFP
Mhariri: Miraji Othman

DW inapendekeza

 • Tarehe 18.07.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11yNz
 • Tarehe 18.07.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/11yNz