1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ponda, Eric4 Novemba 2008

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemteua Rais wa zamani wa Nigeria Olesegun Obasanjo kuwa mjumbe wake maalum katika juhudi za kusaidia kutuliza mzozo mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

https://p.dw.com/p/FnDn
Rais wa zamani nchini Nigeria Olusegun Obasanjo wa pili kushoto, ateuliwa mjumbe maalum kwa mzozo wa Kongo.Picha: dpa


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemteua Rais wa zamani wa Nigeria Olesegun Obasanjo kuwa mjumbe wake maalum katika juhudi za kusaidia kutuliza mzozo mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.




Katibu Mkuu wa Umoja wa Umoja wa Mataifa pia ameandaa ziara kutembelea eneo hilo lenye mzozo mapema iwezekanavyo mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Joseph Kabila na wa Rwanda Paul Kagame katika jitihada za kidiplomasia kutatua mzozo huo.


Uteuzi wa Bwana Obasanjo, ambaye alikuwa Rais wa Nigeria kuanzia mwaka 1999 hadi 2007 kumekuja kufuatia juhudi zaidi za kidiplomasia zinazochukuliwa kuzuia uvamizi unaotaka kufanywa na waasi wanaoongozwa na Laurent Nkunda kuunyakua mji wa Goma.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema Bwana Obasanjo atafanya kazi hiyo kwea kushirikiana na viongozi wa eneo hilo la maziwa makuu na jumuia ya kimataifa ili kulipatia ufumbuzi tatizo hilo la kisiasa.



Aidha amesema pande zote zinazohusika tayari zimeidhinisha uteuzi huo wa Bwana Obasanjo na kuongeza kuwa anategemea Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na wa Ulaya kumuunga mkono.

Akielezea zaidi kuhusu uwezo wa Bwana Obasanjo kushughulikia tatizo hilo Meya wa Mji wa Goma Rodgee Rashid Tumbula amesema ni mtu mwenye uzoefu huo.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema pia Rais Kabila na Rais Kagame wako tayari kukutana na Bwana Obasanjo wiki hii ama mapema wiki ijayo.

Ameongeza kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amepanga kuitisha mkutano wa kanda hiyo mjini Nairobi Kenya, ili kuujadili mzozo huo.


Tayari maelfu ya wakimbizi wameanza kurejea makwao kufuatia kusitishwa kwa mapigano katika muda wa siku tatu zilizopita. Meya huyo alisema kuwa wakimbizi wanaorejea Makwao wanapewa usalama wa kutosha.


Wakati huohuo Waziri Mkuu wa Jamhguri ya Kidemokrasi ya Congo Adolphe Muzito leo ameanza ziara yake mashariki ya nchi hiyo, yenye lengo la kuwatuliza wakazi wa eneo hilo ambao wanakabiliwa na ghasia.


Muzito aliyeteuliwa katika wadhifa huo mwezi uliopita anatarajiwa kuzuru mji wa Goma ambako kuna idadi kubwa ya wakimbizi. Wengi wa wakimbizi hao walikuwa wamepiga kambi katika eneo la Bukavu, iliyoko eneo la Kivu kusini , Kisangani na Dugu.


Mashirika ya kutoa misaada yamekuwa yakisafirisha misaad katika neo hilo la mashariki Mwa Kongo,kuwasaidia maelfu ya wakimbizi hao. Hata hivyo shirika la kutoa misaada la Madaktari wasio na mipaka linasema kuwa misaada zaidi inahitajika katika eneo hilo