1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yaibuka mpaka wa Ugiriki na Uturuki

Lilian Mtono
4 Machi 2020

Mzozo wa wakimbizi unaendelea kufukuta kwenye mpaka kati ya Uturuki na Ugiriki ambao pia ni mpaka kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya, ambako maelfu ya wakimbizi wanataka kuingia barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/3YqAV
Türkei Tränengaseinsatz gegen Flüchtlinge an der Grenze zu Griechenland
Picha: picture-alliance/AA/H. M. Sahin

Wakati huo huo maelfu ya waandamanaji wamekusanyika mbele ya ofisi za kansela wa Ujerumani, Angela Merkel mjini Berlin kushinikiza kufunguliwa kwa mipaka kati ya Ulaya.

Maafisa wa kulinda mpaka nchini Ugiriki wametumia gesi za kutoa machozi mapema hii leo wakati walipokabiliana na wahamiaji wanaolazimisha kuvuka mpaka wake wa ardhini unaoitenganisha nchi hiyo na Uturuki ulioko katika kijiji cha mpakani cha Kastanies.

Jana usiku, waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis amesema kwenye mkutano wa waandishi wa habari pamoja na viongozi wa Umoja wa Ulaya kwenye kijiji hicho cha Kastanies kwamba Ugiriki haikabiliwi na kitisho cha wakimbizi ama tatizo la wahamiaji lakini inakabiliwa na kitisho cha kukosekana kwa usawa.

Mitsotakis amesema watu waliojaribu kuingia Ugiriki katika siku chache zilizopita hawakutokea mkoa wa Idlib nchini Syria, ambao unakabiliwa na mashambulizi ya vikosi vya serikali ya nchi hiyo na washirika wake, Urusi, bali ni wale waliokuwa wanaishi kwa usalama nchini Uturuki na kwa muda mrefu.

Griechenland das Parlament wählt die neue Staatspräsidentin, Premierminister Mitsotakis
Waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis ailaumu Uturuki kwa kujaribu kutishia Umoja wa Ulaya Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Giannakouris

"Kwa hivyo, ni wazi kwamba huu ni ukiukwaji wa tamko la pamoja na Umoja wa Ulaya ambayo iliyosema Uturuki itatakiwa kuwahifadhi wahamiaji nchini mwake na kuzuia njia haramu za kuingia Ugiriki. Kwa bahati mbaya Uturuki imekuwa mfanyabiashara rasmi wa wahamiaji haramu katika Jumuiya ya Ulaya. Tatizo lililopo sasa si wamibizi ama wahamiaji ila ni kitisho cha kukosekana kwa usawa kwenye mipaka ya Ugiriki ambayo pia ni mipaka ya Ulaya." alisema Mitsotakis.

Alisema Umoja wa Ulaya hautakubali kutishiwa na Uturuki kufuatia mzozo huu wa wahamiaji na kusisitiza kuwa wako tayari kushirikiana katika kukabiliana na tatizo la wakimbizi lakini pia kusaka suluhu ya changamoto iliyopo Syria ingawa si chini ya mazingira yaliyopo. Amesema wajibu wake ni kulinda uhuru wa taifa lake.

Deutschland Tausende demonstrieren vor dem Kanzleramt für Grenzöffnung
Waandamanaji walioandamana mbele ya ofisi za kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kushinikiza kufunguliwa mipakaPicha: Imago-Images/J. Große

Huku hayo yakiarifiwa, takriban watu elfu tatu wamekusanyika mjini Berlin, huku maandamano kama hayo yakifanyika pia katika mji wa Hamburg na Potsdam, hii ikiwa ni kulingana na vyombo vya habari vya Ujerumani.

Kundi linalojiita "Seebrucke" ama "Daraja la Bahari" lililoongoza maandamano hayo limeandika kupitia mtandaoni kwamba linasimama dhidi ya sera za kufunga mipaka ya Umoja wa Ulaya na kutaka kufunguliwa kwa mipaka hiyo. Seebrucke limesema linataka njia salama na kukomeshwa vitendo vya jinai kwenye meli zinazowaokoa wahamiaji baharini.

Maandamano hayo yameandaliwa katika wakati ambapo wahamiaji wamekusanyika kwenye mpaka kati ya Ugiriki na Uturuki baada ya rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kutangaza wiki iliyopita kwamba nchi yake haitaendelea kuwazuia wahamiaji kuvuka mpaka na kuingia mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Chini ya makubaliano ya mwaka 2016 kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya kuhusu wakimbizi, pande zote mbili zilikuwa zikishirikiana kuwazuia wahamiaji kuvuka mpaka na kuingia Ulaya kutokea Uturuki. Hapo jana waandamanaji waliyaelezea makubaliano hayo kama "sumu" huku wakipiga kelele wakisema "tuna nafasi" . Polisi inasema idadi ya waandamanaji hao ilikadiriwa kuwa 3,500 wakati waratibu wa maandamano wakisema ilikuwa zaidi ya 8,000.

Mashirika: APE/DW