Maoni:Hakuna amani ya Olimpiki Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.08.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maoni:Hakuna amani ya Olimpiki Ukraine

Je, Urusi inapania kuishambulia Ukraine katika vita kamili kuanzisha daraja hadi Crimea? Hapana, rais wa Urusi Vladimir Putin anacheza mchezo tofauti na taifa jirani, anaandika Christian F. Trippe katika maoni yake.

Ubalozi wa Urusi mjini Kiev hauna watu, wanadiplomasia wameondolewa na ni maafisa wa usalama pekee waliobakia: Hivi karibuni tu uteuzi wa balozi mpya wa Urusi nchini Ukraine haukufaulu kwa sababu serikali ya Ukraine ilitia guu. Urusi, kwa kulipiza kisasi, haijaona balozi yeyote kutoka Ukraine kwa miezi kadhaa. Kwa maana hiyo hakuna uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili kwa sasa - ingawa hakujawahi kuwa na kitu kama kusitisha rasmi mahusiano.

Vita vikubwa vyanukia?

Watu ambao wana wasiwasi watauchukulia mkwamo huu wa kidiplomasia kama ishara ya vita vikubwa vinavyonukia kati ya nchi hizo mbili. Kweli kuna viashiria kadhaa: mapigano katika eneo lililotengwa katika eneo la mashariki ambako hakutakiwi kuwa na shughuli za kijeshi, yanaendelea kuongezeka na kuwa makali wiki hadi wiki; mkataba wa kusitisha mapigano wa mjini Minsk umefujwa na kuwa kama zoezi la karatasi iliyolowa damu. Waangalizi wanaripoti kwamba silaha zaidi nzito nzito zinaendelea kupelekwa katika eneo la mapigano.

Pia wataalamu wa masuala ya kijeshi nchini Urusi na katika mataifa wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO wanadokeza juu ya vikosi vikubwa vya Urusi kutembea katika eneo la mpakani. Kwa maneno mengine ni wanajeshi kujikusanya upya au wanajeshi kutumwa. Maneno yote haya yanatisha.

Trippe Christian F. Kommentarbild App

Christian Trippe, Mwandishi wa DW mjini Kiev

Fauka ya hayo:idara ya ujasusi ya Urusi, FSB inadai imezima shambulizi la kigaidi la Ukraine katika rasi ya Crimea; Warusi wawili wanaripotiwa kuuliwa kufuatia uvamizi huo unaodaiwa kufanywa na Ukraine. Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa haraka alipitisha uamuzi kwamba sasa hakutakuwa tena na mazungumzo zaidi ya ngazi ya juu kuhusu mkataba wa Minsk. Je, Urusi inatafuta tu kisingizio kuishambulia Ukraine?

Je, vita vya Urusi dhidi ya Georgia, miaka minane iliyopita, havikuzuka mwezi Agosti pia? Je michezo ya Olimpiki haikufanyika wakati huo pia - jambo ambalo liliitatiza jamii ya kimataifa? Je nchi za magharibi hazionekani kuwa kilema na kushindwa - huku Marekani ikiwa imezama katika kampeni za uchaguzi wa urais, na viongozi wa Ulaya wakiwa wamedhoofishwa?

Lini, kama sio sasa? Hilo ni swali ambalo viongozi wa utawala wa Kremlin wenye misimamo mikali huenda wakajiuliza wenyewe, na hivyo kuziachia huru fikra zao za utanuzi. Kutoka kwa mtizamo wao wa kibeberu - ambao unajumuisha Dola kuu ya Urusi - kutwaliwa kwa rasi ya Crimea na msaada wa kijeshi kwa waasi katika eneo la Donbass, bila shaka haliwezi kuwa neno la mwisho katika historia ya dunia.

Kuchafua sherehe ya Siku ya Uhuru

Kwa kuzingatia mazingira ya sasa na hali ya mapigano mashariki ya Ukraine yote haya yanajumuisha mchanganyiko unaoonekana zaidi kama vita. Ni mchanganyiko uliopikwa Kremlin ambao mvuke wake unaibua wasiwasi na hofu kubwa mjini Kiev na kusababisha kichefuchefu katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin na katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris.

Rais Putin, kwa kuzingatia nguvu za jeshi lake, bila shaka anataka kuchukua udhibiti wa michakato yote hii ambayo kwa haraka huenda ikaamua mustakabali wa Ukraine. Uongozi wa Urusi, hata hivyo utapoteza nafasi hii ya madaraka iwapo itaamua kuingia katika vita vya wazi kwa ajili ya kipande cha ardhi mashariki ya Ukraine. Kwa njia hiyo vikwazo vya mataifa ya magharibi vitaimarishwa zaidi na kuudhoofisha zaidi uchumi wa Urusi.

Kwa maana hiyo Urusi pengine itaendelea kutumia vitisho. Agosti 24, Ukraine inaadhimisha siku ya uhuru kutoka kwa Urusi kwa robo karne sasa. Watawala wa Kremlin wanataka kuhakikisha kwamba sherehe hizi zinavurugwa kikamilifu na raia wa Ukraine.

Je una la kuongezea? Andika maoni yako hapo chini.

Mwandishi:Trippe, Christian F

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com